Abiria Moshi wasotea usafiri, nauli juu - EDUSPORTSTZ

Latest

Abiria Moshi wasotea usafiri, nauli juuBaadhi ya abiria wakiwa katika eneo la Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi, baada ya kukosa usafiri wa kwenda maeneo waliyokusudia. Picha na Dionis Nyato
Moshi. Shida ya usafiri kutoka mkoa wa Kilimanjaro kwenda Mkoa wa Arusha nyakati za jioni umefanya baadhi ya wasafirishaji kupandisha nauli kutoka Sh2,500 hadi Sh5,000.

Adha hiyo imesababishwa na uchache wa magari, hivyo kusababisha abiria kuwa wengi katika kituo cha mabasi cha Moshi Mjini.

Abiria wanaotokea Wilaya ya Rombo nao wanalazimika kulipa Sh5,000 kutokea Mkuu badala ya Sh3,000.

Wakizungumza na Mwananchi jana, wasafiri hao walieleza kuwa madereva wa mabasi madogo ‘coaster’ na noah wamekuwa wakiwanyanyapaa barabarani pale wanapokuwa na pungufu ya nauli wanayoitaka.


 
Anna Shirima, aliyekuwa akisafiri kutoka Rombo eneo la Mkuu kwenda Moshi Mjini, alisema kuwa wamekuwa wakikaa vituoni kwa muda mrefu kutokana na magari mengi yanayoingia stendi kukataa kuwabeba kwa sababu ya kuzidishiwa nauli kutoka Sh3,000 hadi Sh5,000.

“Tunapowauliza kwa nini wanatupandishia nauli hawaongei na tunapowaomba tiketi ya hiyo nauli kubwa wanayotutoza wanagoma, kwa hiyo ndio hivyo watu wanajikuta wanapanda noah kwa hiyo nauli, maana unakuta mtu hana chaguo jingine kwa sababu ni lazima asafiri,” alisema

Amosi Njau, aliyekuwa akisafiri kutoka Moshi Mjini kwenda Arusha alisema kutokana na ukosefu wa usafiri, baadhi ya watu hulazimika kurudi walikotoka.


“Mimi niko hapa stendi lakini sina uhakika wa kusafiri, angalia watu walivyojazana hapa stendi, yaani wakati wa jioni ni tabu, tunahaha hapa stendi magari ni machache abiria ni wengi, wakati mwingine watu wanagombania magari hadi wengine wanapitia madirishani,” alisema Njau.

Akizungumza, Msimamizi wa kituo cha Mabasi Mjini Moshi, Samwel Mlay alikiri kuwepo kwa wingi wa abiria katika stendi hiyo, ambao alisema stendi hiyo ina mabasi madogo zaidi ya 180, lakini bado changamoto ya abiria ni kubwa.

“Ni kweli kumekuwa na changamoto ya usafiri katika stendi ya mabasi hapa Moshi Mjini, sasa hivi kumekuwa na changamoto hasa kwa watu wanaotoka katika Wilaya ya Rombo kuja Moshi mjini na sehemu nyingine mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro ambapo watu wengi wanakuja hapa katikati ya mji ambapo ndio kituo kikubwa cha mabasi kwa ajili ya kwenda mikoani,” alisema Mlay.

“Licha ya kuwepo kwa treni katika mkoa wa Kilimanjaro, bado changamoto ya usafiri ni kubwa kutokana na wingi wa abiria waliopo, abiria wamekuwa ni wengi kuliko vyombo vya usafiri vilivyopo,” alisema na kuongeza:


 
“Tarehe 25 hadi 30 Desemba mwaka jana, Latra waliruhusu coaster zikawa zinatoa watu kutoka Dar es Salaam kuja huku, kwa hiyo sasahivi naona na vyema Latra waruhusu coaster zitoke Kilimanjaro kupeleka watu Dar es Salaam, kwani abiria ni wengi sana katika stendi ya Moshi,” alisema Mlay.

Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra) Mkoa wa Kilimanjaro, Paulo Michael aliwataka abiria wote wanaotozwa nauli kubwa kinyume na nauli elekezi ya mamlaka hiyo watoe taarifa ili wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua.

“Tangu asubuhi tuko hapa stendi na kama kuna gari ambalo linatoza nauli kubwa kwa abiria wanaosafiri kwenda kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini,abiria usisite kutoa taarifa, toa taarifa ili tuweze kuwashughulikia hawa wanaotoza nauli kinyume na sheria,” alisema Paul.

Alisema Latra imekuwa ikitoa adhabu kwa wasafirishaji wanaopandisha nauli kila wanapobaini lakini wanahitaji taarifa zaidi kutoka kwa abiria
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz