Taarifa kutoka ndani Young Africans ni kwamba kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi kawasilisha mapema ripoti kwa mabosi wa klabu hiyo ikiwa ni mikakati ya kuanza kukisuka upya kikosi cha msimu ujao.
Hesabu za Gamondi zimeonyesha kuhitaji kuongeza kipa mmoja atakayechukua moja ya nafasi ya makipa watatu waliopo sasa akiwamo Djigui Diarra, Metacha Mnata na Aboutwalib Mshery. Mmoja kati ya hawa atapewa mkono wa kwaheri.
Kwenye ukuta hasa eneo la mabeki ripoti hiyo imeonyesha kuhitaji beki mmoja wa kushoto ambapo hapa kuna uwezekano mkubwa kwa mkongwe Joyce Lomalisa akapewa mkono wa kwaheri kwani mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Ripoti hiyo, inaelezwa pia inahitaji kiungo mkabaji mwenye ubora zaidi au sawa na Khalid Aucho atakayejiunga kikosini kusaidiana na Mganda huyo pamoja na Jonas Mkude aliyepindua meza kibabe kwa kubakishwa baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye mechi mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Gamondi pia inaelezwa anahitaji winga mmoja na mshambuliaji wa maana watakaokuja kuongeza nguvu kwenye eneo la mwisho ambalo bado mshambuliaji Joseph Guede ameanza cheche akifunga dhidi ya Singida Fountain Gate.
No comments:
Post a Comment