Mambo ya Kufanya Unapokuwa Kwenye Stresi za Mapenzi! - EDUSPORTSTZ

Latest

Mambo ya Kufanya Unapokuwa Kwenye Stresi za Mapenzi!

Mambo ya Kufanya Unapokuwa Kwenye Stresi za Mapenzi!

NI nadra sana mtu kuishi miaka yote hapa duniani bila kuingia kwenye ‘stresi’ za mapenzi. Nyakati kama hizi kwa wapendanao lazima wazipitie. Unaweza kuwa ndiyo kwanza umeingia au hata katikati ya safari yenu, utakutana na stresi tu.

Stresi zipo tu kwa sababu wahusika kwenye uhusiano ni binadamu. Mnakutana mwanaume na mwanamke ambao mmekulia kwenye familia tofautitofauti. Mnapokuwa pamoja lazima mpishane, mtofautiane na hata mgombane.

Hayo ndiyo maisha ya uhusiano. Huwezi kukwepa stresi zinapokuja huwa ni kama ajali. Unakuwa hujazitarajia, lakini zinatokea tu. Lazima tuelewe tunapokuwa kwenye stresi siku zote mambo hayawezi kuwa sawa.

Mbali na uhusiano, lakini hata kwenye maisha ya kawaida. Kwenye nyakati hizi ndipo watu wanapofanya mambo tofauti na matarajio yao. Kama ni kazi, kama ni biashara, anaweza kujikuta ameharibu mambo kwa sababu tu ya stresi za uhusiano.

Kuna watu huwa wenyewe ni kama vile stresi ni sehemu ya maisha yao. Yaani badala ya kujitahidi kutoka kwenye kipindi hicho, wao wanazidi kukuongezea. Kichwa chako kitajaa mawazo mpaka kukaribia ‘kupasuka’.

Sasa unapokuwa kwenye nyakati hizi, unatakiwa kujua namna ya kujitoa kwenye mawazo hayo ili maisha ya kawaida yaendelee. Ukishindwa kujitoa na kuendelea na maumivu hayo kwa muda mrefu, unaweza kupata madhara makubwa zaidi yanayoweza hata kugharimu uhai wako.

Watu wanakufa kwa sababu ya stresi za mapenzi. Wengine hujikuta wameua kutokana na stresi hizi za mapenzi. Ndiyo maana leo nasisitiza hapa kwenye makala haya, kwa namna yoyote ile hakikisha unajitoa kwenye stresi.

Kwa kawaida wapendanao mnapokutana, huwa mnakuwa na dhamira moja. Mnahitaji kufika mbali kwenye safari yenu. Hii ni dhamira ya wengi japo wapo wengine ambao wao hawana huo mpango, wanataka tu kuishi kwa muda fulani, basi wahamie kwingine.

Lakini kwa wale ambao naamini lengo lao ni kufika mbali, lazima watambue kwamba kama nilivyosema awali, ni binadamu hivyo stresi zitakuja, lakini wasikubali zikaishi muda mrefu. Kila mmoja aone ana wajibu wa kuziondoa pale zinapotokea na si kuziongeza.

Hivyo basi, unapoingia kwenye stresi wewe usipaniki. Unachotakia kufanya ni kuifanya akili yako tu iamini kwamba suala hilo limekuja kwa bahati mbaya na wewe na mwenza wako ndiyo wenye jukumu la kuliondoa.

Kama kuna shida kati yenu, hakuna sababu ya kugombana. Ninyi mnapeana nafasi nzuri ya kulitafakari. Kila mmoja aone kwamba maisha yenu yana thamani zaidi kuliko hizo stresi. Hivyo pale mlipokoseana, zungumzeni kwa lugha nzuri na kila mmoja wenu aone ana sababu ya kujishusha.

Kusikilizana ndiyo kila kitu kwenye uhusiano. Asiwepo mtu anayejiona yupo juu zaidi ya mwenzake. Zungumzeni na wote muwe tayari kumaliza tatizo. Ukiona mwenza wako anakuwa na mtazamo hasi tu katika kutatua tatizo jua huyo ana jambo lake, hayupo pamoja na wewe kifikra.

Jitahidi sana kuzungumza na mwenza wako, lakini ukiona hakuelewi, wewe usigombane naye. Ipe nafasi akili yako iwaze mambo mengine. Ukiona baada ya kupita kipindi kirefu kupita na mwenzako hataki kurudi kwenye maisha ya kawaida, vyema ukaachana naye.

Utaumia kwa muda, lakini ni heri kujitoa kuliko kuishi kwenye mateso ya muda mrefu. Thamani ya uhai wako ni kubwa kuliko kitu kingine. Chagua kulinda uhai wako na hata wa kwake pia. Unaweza kulazimisha na kujikuta umefanya tukio la mauaji, bora kuishi maisha yako na kama ni mpenzi utampata mwingine.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

Edusportstz