Miongoni mwa stori zinazo make headlines kwa sasa kwenye tasnia ya soka ni sakata la mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ambaye aliomba kuvunja mkataba na klabu yake hiyo kwa kile alichoeleza kuwa anataka kwenda sehemu nyingine kutafuta changamoto nyingine lakini Azam wakaweka masharti mazito.
Azam walidai kuwa mchezaji huyo ana mkataba nao mpaka mwaka 2026 hivyo wakataja kiasi kikubwa cha pesa ambacho ni dola 300,000 ili kuvunja mkataba huo ama kama kuna klabu inamtaka basi ipeleke ofa mezani.
Zipo klabu mbalimbali Tanzania nan je ya Tanzania ikiwemo Simba, Yanga, Al Hilal ya Sudan ambao walipeleka ofa zao kwa matajiri hao wa Dar lakini mwisho wa siku biashara na mchezaji huyo haikuweza kufanikiwa mpaka sasa jambo ambalo Dube alisisitiza kuwa hataki kuuzwa bali anataka kuwa huru na yeye atachagua pa kwenda kucheza.
Baada ya kuona amebaniwa, aliamua kufikisha malalamiko yake kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF akiwa na ombi moja tu la msingi ambalo ni kuiomba TFF itambue kuwa mkataba wake unaishia 2024 na sio 2026 kama Azam wenyewe wanavyodai.
Jana ilikuwa siku ya kusikiliza shauri hilo ambapo kamati ya TFF ilisikiliza hoja za pande zote mbili na kupokea vielelezo vyao ambapo kila mmoja anaamini ana haki kwenye kile anachokisimamia, huku ikitoa maelezo kuwa itataja siku maalum ya kutoa maamuzi hayo.
Baada ya hapo, Wakili wa Dube, Respicius Didad ambaye ameeleza kesi ya msingi na madai yao wamesimamia wapi.
"Ombi la mchezaji limeskilizwa na suala linahusu mikataba, baada ya kusikilizwa pande zote, kamati imesema itatujulisha siku ya maamuzi baada ya wao kujadili na kutoa maamuzi lakini kesi imesikilizwa, imemalizika na tunasubiri maamuzi.
“Prince Dube anasema ana mkata na Azam unaoisha Julai 31, 2024 lakini Azam wanasema wao mkataba mwingine unaoisha Julai 2026, hicho ndicho kinachobishaniwa humo ndani, vielelezo vyote vimewasilishwa. Tunaamini kamati itatenda haki.
“Siwezi kusema kama mkataba upo TFF au haupo, kamati ndiyo italiongelea hili lakini tunachosema sisi ni kwamba mkata ambao anao Prince Dube na Klabu yake ni mkataba unaoisha Julai 31, 2024.
“Mgogoro umeanza na upo unasikilizwa kwa hiyo huwezi kusema kwa nini haukuwa kabla au baada, suala la msingi ni kwamba mgogoro umekuja, upo ndani ya muda na tunasubiri maamuzi.
“Sisi hatuhitaji mkataba mpya, tunataka TFF itambue kwamba mkataba ambao Prince Dube amesaini na Azam unaishia Julai 31, 2024. Maamuzi yakishatolewa ndiyo tutajua tunafanya nini, huwezi kuvuka daraja kabla hujalifikia,” amesema wakili Didas.
DUBE AFUNGUKA Dube hakuwa mtu mwenye maneno mengi, alisema, “Tusubiri kuona nini kitatokea, naamini kila kitu kitaenda vizuri.” Kwa upande wa mwanasheria wake, Didas amesema anaamini kamati itatenda haki kwa mteja wake.
Upande wa Azam FC wao wanasema mkataba huo unaisha 2026 jambo ambalo linaleta mkanganyiko na ndicho kiini cha mgogoro huo mpaka kufikishana TFF.
Meneja Idara ya Habari ya Azam FC, Zakazakazi amesema; “Mkataba wake ulikuwa unaisha Julai 2024 na mara tu mkataba wake ukiisha ndio mkataba huu mpya utaanza kufanya kazi hadi 2026.
“Mkataba wa mchezaji kama unakuwa unafika tamati 2025 halafu ukaongeza mwingine hadi 2028 kwa mfano, huo mpya hauwezo ukaingia kwenye system hadi huo wa 2025 uwe umeisha ndiyo utaratibu wa mifumo ya usajili wa wachezaji.
“Kwa hiyo mkataba unaoisha 2024 ndiyo ambao upo kwenye mfumo lakini ule unaoisha 2026 usingeingia mpaka huu wa 2024 uishe,” amesema Zakazakazi.
Kwa maelezo ya hayo ya Azam FC inaonekana mkataba unaoishia 2026 walishakaa mezani wakakubaliana na wakasaini na mchezaji lakini ahujaingizwa kwenye mfumo wa TFF mpaka ule wa awali utakapoisha, hivyo mkataba huo unaoishia 2026 haupo TFF.
Kiutaratibu, kutokuwepo kwa mkataba huo kwenye mfumo hakufuti uhalali wa mkataba huo kwa sababu mkataba ni makubaliano ya pande mbili na kama vielelezo vinajitosheleza, kuwepo kwenye mfumo ni suala jingine.
Dube na kambi yake wao wamesimama kwenye unaoishia 2024 lakini huu wa 2026 hawautambui, hivyo Azam wana kazi ya kuishawishi TFF kwa vielezo kuwa mkataba ule ni halali na upande wa Dube wana kazi ya kuishawishi TFF kwa vielezo kuwa mkataba ule sio halali.
Utakumbuka sakata la Bernard Morrison na Yanga lilikuwa kama hili la Dube na Azam, baada ya Morrison kugundua kuwa mkataba aliosaini na Yanga haupo TFF akaamua kutoutambua, na mwisho wa siku alicheza karata zake kwa makini akashinda.
Kwenye sakata hilo, TFF ilibaini kuwa Morrison alisani mkataba kweli na Yanga lakini mkataba ule ukawa na mapungufu, na mwisho wa siku Morrison aliruhusiwa kwenda Simba SC, jambo hili linaweza kujirudia pia kwa Dube na Azam.
Lakini hata sakata la Fei Toto na Yanga lilianza hivi hivi, mchezaji anataka kuondoka lakini ana mkataba na timu yake, mambo yakaenda yakarudi mwisho wa siku Rais Samia Suluhu akaingilia kati, Fei Toto akawa ameruhusiwa kuondoka Yanga.
Tusubiri maamuzi ya TFF tuone nani atakuwa na haki kwenye sakala hili, Prince Dube ambaye anasema mkataba wake unaisha Julai 2024, ama Azam FC wanaosema mkataba unaisha Julai 2026.
No comments:
Post a Comment