KESI YA SABAYA: Shahidi asema alimpokea diwani akivuja damu - EDUSPORTSTZ

Latest

KESI YA SABAYA: Shahidi asema alimpokea diwani akivuja damu

 


Arusha. Dk Ngiana Mtui (28),   shahidi wa 10 wa Jamhuri katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili   ameieleza mahakama kuwa alimpokea na kumpatia matibabu Bakari Msangi.

Shahidi wa 10 wa Jamhuri katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili, Dk. Ngiana Mtui (28)  ameieleza mahakama kuwa alimpokea na kumpatia matibabu Bakari Msangi.

Amedai kuwa wakati akimpokea Msangi ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini akiwa na majeraha usoni, ngozi ikiwa na alama nyekundu huku akiwa amevimba sikio la kulia lililokuwa limevilia damu.

Akitoa ushahidi wake leo Agosti 10,2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, Dk. Ngiana kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mt. Meru ameieleza mahakama kuwa majeraha hayo yalisababishwa na kupigwa na kitu butu usoni huku akilalamika kuwa na maumivu .

Ameeleza kuwa baada ya kupatiwa matibabu alipumzishwa kwa muda wa dakika 20 kabla ya kuruhusiwa.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Baraka Mgaya, ameeleza kuwa baada ya kumpatia matibabu Februari 2,mwaka huu, alijaza fomu namba tatu (PF 3) na kuihifadhi ambapo huwa zinakwenda kuchukuliwa na polisi hospitalini hapo.

"Alikuja akiwa analalamika maumivu makali zaidi eneo la masikio yote mawili, pande za uso na ngozi yake ilikuwa nyekundu sehemu nyingi. Kwa upande wa sikio la kulia lilikuwa limevimba na kulikuwa na damu imevulia ndani kwenye mfupa wa ndani ya sikio na michubuko midogo," amesema na kuongeza.

"Tulimpatia huduma ya kwanza ikiwemo kumchoma sindano ya diclofenac kwa ajili ya kupunguza maumivu aliyolalamika kuwa nayo na katika sehemu zenye michubuko tulipaka dawa ili kuzuia na kuua bakteria kisha tukampa kitanda apumzike kuruhusu dawa ifanye kazi kwa muda wa kama dakika 20."

Ameendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya PF3 kujazwa na yeye kama daktari fomu hiyo ilichukuliwa na polisi mwezi Machi, mwaka huu na aliyechukuwa hamfahamu kwa kuwa sio kazi yake na uchukuaji wa fomu una taratibu za kuzichukua.

Shahidi huyo alidai kuwa taarifa za wagonjwa hospitalini hapo zinawekwa kwenye mfumo wa kielektroniki na kuwa PF 3 ilijazwa Februari 10,2021.

Akihojiwa na Wakili wa utetezi Mosses Mahuna, shahidi huyo alidai siku ya tukio alikabidhiwa PF 3 hiyo na moja ya ndugu wa Msangi na kuwa amejaza PF 3 mbili za mgonjwa huyo na hajui PF 3 ya Februari 10 mahali ilipo.

Akihojiwa na Wakili Dancan Oola, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa licha kujaza PF 3 ya kwanza, Machi 10 mwaka huu alipelekewa PF 3 nyingine aliyopaswa kuijaza ambapo alichukua kwenye mfumo maelezo aliyokuwa ameijaza katika PF 3 ya awali na kuwa hakumbuki jina la aliyeleta kwani, majina huandikwa kwenye kitabu maalum kilichopo hospitalini hapo.

Sabaya na wenzake wawili wanashitakiwa kwa makosa matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha.

Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz