BREAKING

Search here

TUFOLLOW UWE MIONGONI MWA WANAOTUMIWA HABARI KILA SIKU

Friday, 28 July 2017

Unafahamu kwanini HIFADHI YA KITULO inaitwa“Bustani ya Mungu”

Image result for hifadhi ya kituloImage result for hifadhi ya kituloHifadhi ya kitaifa ya Kitulo, ipo katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, ikiwa
katikati ya safu za milima ya Uporoto, Kipengule na Livingstone. Ina ukubwa wa kilometa za mraba 412 ambazo ni sawa na maili za mraba 159.4.

Sehemu kubwa ya hifadhi hii ambayo kama zilivyo hifadhi zingine nchini Tanzania, inasimamiwa na kuratibiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imetapakaa katika mikoa miwili ya Mbeya na Njombe.
 Eneo tengefu la hifadhi hii, limejumuisha safu za Kitulo na sehemu ya safu za milima ya Livingstone, ikiwa ni hifadhi ya kwanza kabisa kutambulika katika ukanda wa Kitropiki katika Afrika, kuwahi kuanzishwa kwa minajili ya utunzaji wa mimea asilia ambayo sehemu kubwa ni maua.
Ikiwa inaitwa kwa jina la utani la "Bustani ya Mungu", na wenyeji wa maeneo ya jirani, hifadhi hii pia imekuwa ikijulikana kwa jina maarufu la "Serengeti ya Maua", jina ambalo lilibatizwa hifadhi hii kutoka kwa wageni hususan walio wataalamu wa maua, waliokuwa wakiitembelea kutoka nje ya nchi.

Wazo la kuwepo kwa hifadhi hii, lilianzishwa na Asasi yenye kujihusisha na utunzaji wa wanyama na uoto asilia ya Wildlife Conservation Society (WCS), baada ya jopo la wataalamu kutoka asasi hii kuanza kuguswa na ukuaji wa biashara ya mimea asilia ambayo ipo katika hifadhi hii peke yake, sanjari na kuzidi kushamiri kwa shughuli za uvuvi katika maeneo ya jirani na eneo hilo. Na mwaka 2002, aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, enzi hizo, akatangaza uanzishwaji wa hifadhi hii ya Kitulo

Mwaka 2005, ilitangazwa rasmi katika gazeti la serikali na kuwa hifadhi ya 14 ya taifa, na zipo taarifa kuwa, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limekuwa likipigania hifadhi hii ya Kitulo, kujuisha pia mapori yaliyoko karibu ya kwenye safu za milima ya Rungwe.

Hifadhi ya Kitulo, ina aina mbalimbali za mimea ipatayo 350, ambazo zimeshaandikishwa rasmi hadi sasa, ikiwa ni pamoja na aina 45 za mimea inayojulikana kitaalamu kwa jina la "Orchids", ambayo kimsingi haipatikani sehemu nyingine yoyote ile duniani, zaidi ya kwenye hifadhi hii tu.

Kati ya hizo, aina hizo za mimea, 31 zinaweza kupatikana pia katika sehemu kadhaa za Tanzania, aina 25, zikiwa zinapatikana katika ukanda wa hifadhi hii huku aina takriban tatu zikiwa zinapatikana kwenye eneo la hifadhi pekee.

Hifadhi hii pia ni maarufu kwa uwepo wa ndege aina kadhaa ambazo pia hazipatikani kwa urahisi katika sehemu zingine duniani, miongoni mwao wakiwemo ndege wanaojulikana kwa majina ya kitaalamu ya Blue swallow, Denham’s bustard, Mountain marsh widow, Njombe cist cola pamoja na Kipengere seedeater. Aidha, hifadhi hii pia ni maarufu kwa kuwa na aina kadhaa za mijusi, vyura na vinyonga, ambao pia hawapatikani kwa urahisi sehemu zingine duniani.

Licha ya ukweli kuwa, hifadhi hii imekuwa haipewi uzito katika kutangazwa au kuelezewa sifa zake kwa wenyeji na hata wageni, kiasi cha kuifanya isiwe maarufu sana ndani na nje ya Tanzania, Kitulo, bado ni hifadhi ambayo kwa hakika inamfanya mtembeleaji wake kufurahia kila hatua ambayo anaifanya ndani ya eneo la hifadhi, huku akiwa halazimiki kukaa na kuzunguka kwa gari kwa dakika au hata saa kadhaa kabla ya kuona ubora wa hifadhi yenyewe.

Na ukiachilia mbali tatizo la miundombinu ya kufika eneo hilo kuwa sio ya ubora wa hali ya juu, bado ni rahisi sana kufika katika hifadhi hii, ambayo iko umbali wa takriban kilomita 100 tu kutoka yalipo makao makuu ya Mkoa wa Mbeya.

Hakuna mabasi rasmi yenye kufika sehemu hiyo ya hifadhi, na kwakuwa hata mkoa wa Mbeya wenyewe haujawa na mwamko sana katika masuala ya utalii, kampuni pekee yenye kuweza kutoa huduma za kufika katika hifadhi hiyo ni ile ya Gazelle Safaris, ambayo ina makao yake makuu jijini Mbeya.

Hata hivyo, licha ya ukiwa wake huu, kwa wale wenye kupenda kushuhudia mandhari za kupendeza, zenye mchanganyiko wa rangirangi za mimea, na uchanuaji wa maua ambao huleta mvuto wa kipekee pindi unapoendelea, Kitulo, ni hifadhi ambayo ukiitembelea katika miezi ya kati ya Novemba na April, utaishia kustaajabu ni namna gani imeshindikana kuwa moja ya vivutio vyenye kujulikana sana ndani na nje ya Tanzania.

Kama ambavyo imetanabaishwa awali, hifadhi hii ni kama imeachwa ukiwa kwani hata huduma za malazi si za uhakika sana katika maeneo ya karibu, ukiachilia mbali hoteli kadhaa za hadhi ya kawaida zenye kumilikiwa na wenyeji wa maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment