Maajabu:Ndege warukao kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kitulo hadi Ulaya - EDUSPORTSTZ

Latest

Maajabu:Ndege warukao kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kitulo hadi Ulaya



By edusports
Hifadhi ya Taifa Kitulo ndiyo eneo pekee Tanzania lenye ndege aina ya tandawala machaka (Denhams Bustard) wenye uwezo wa kuruka kutoka bara moja hadi jingine
Hifadhi hiyo inayopita katika mikoa ya Mbeya na Njombe ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005 ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo, msitu wa Livingstone na bonde la Numbi.
Kitulo ina ukubwa wa kilometa za mraba 442. Awali ilijulikana kama Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredirick Elton kupita eneo hilo mwaka 1870. Mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hilo kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa kondoo.
Kutokana na umuhimu wa eneo hilo wadau mbalimbali wa mazingira walipendekeza eneo litangazwe kuwa hifadhi ya Taifa ili kulinda umaridadi wa maua, ndege na mimea adimu inayopatikana ndani ya eneo hili.
Dk. Ezekiel Dembe, kaimu mkurugenzi wa Mipango ya Maendeleo na Huduma za utalii katika Hifadhi ya Kitulo anasisitiza kuwa ndege aina ya tandawili machaka hawapatikani sehemu nyingine yoyote hapa Tanzania zaidi ya Kitulo.
Watalii na watafiti wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani hufika katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa ajili ya kuwaona ndege hawa ambao wanasafiri umbali mrefu wa kutoka bara moja kwenda bara jingine. 
Dk Dembe anasema ndege hao adimu wanapendwa na watalii wengi duniani na kwamba hifadhi hiyo ndiyo eneo pekee ambalo ndege hao hutaga mayai na kuzaliana kwa wingi kabla ya kusafiri kwenda mabara mengine.
“Utafiti unaonyesha kuna ndege aina ya tandawili machaka ambao waliwekwa alama walipokuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo na baadaye kuonekana wakiwa na alama zao katika hifadhi moja Australia. Utafiti huu ndiyo uliothibitisha kuwa ndege wa aina hiyo wanasafiri kwa kuruka kutoka bara moja kwenda jingine,’’ anasema mhifadhi huyo.
Ndege hao wamekuwa na tabia katika msimu fulani kuruka na kufika katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa ajili ya kutaga mayai na kuangua vifaranga kutokana na mazingira ya hifadhi hiyo kuonekana kuwa ni mahali pekee duniani penye hali ya hewa rafiki kwa ndege hao kuzaliana. Hivyo baada ya kutaga mayai, kuangua vifaranga na ndege kukua, huruka na kwenda mabara mengine duniani.
Utafiti umebaini kuwa katika Hifadhi ya Kitulo ndege aina ya abdims stock, denhams (tandawili machaka) na blue swallow ambao wametoka Afrika Kaskazini, Afrika Kusini, Australia na Ulaya wanaitumia Hifadhi ya Kitulo kama makazi yao katika misimu tofauti.
Watalii wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kitulo wanaweza kuangalia ndege adimu katika Ziwa Zambwe na misitu, kuweka kambi kwa ajili ya malengo mbalimbali, utalii wa kutembea kwa miguu, kupanda farasi, michezo ya gofu na kukwea milima.
Licha ya ndege adimu waliopo, Hifadhi ya Kitulo pia inasifika kwa kuwa na zaidi ya aina 40 za maua mbalimbali ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote duniani.
Unapoingia katika hifadhi hiyo msimu wa maua kuchanua inakuwa kama vile unga umeanikwa katika miinuko ya hifadhi hiyo hali ambayo inaongeza mvuto kwa watazamaji.
Hifadhi hii imejaliwa kwa kuwa na aina zaidi ya 350 ya mimea ya jamii ya flora.
Mhifadhi Godwel Ole Meing’ataki, Mratibu wa Miradi, mipango ya maendeleo na uboreshaji huduma ya vivutio vya utalii kusini, Spanest anasema katika hifadhi nyingine kuna ujangili, tofauti na Hifadhi ya Kitulo ambako ujangili wake ni wa viazi vya asili (vikanda) ambavyo huchimbwa na kuuzwa nje ya nchi kwa bei kubwa.
Yapo mengi ya kujivunia katika Hifadhi ya Kitulo ukiwamo uwanda wa tambarare, mabonde, vilima na maporomoko ya maji kama Numbi ambako ndani ya msitu kuna miti ya aina ya cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiriwa kuwa ndiyo miti mirefu kuliko yote duniani.
Hifadhi ya Kitulo inafikika kwa gari kutoka Chimala, kilometa 78 Mashariki mwa mji wa Mbeya. Unapanda milima yenye kona 68 ambayo pia ni kivutio hadi katika mji wa Matamba wilayani Makete Mkoa wa Njombe.
Reli ya Tazara hupita karibu na Hifadhi ya Taifa ya kitulo. Pia unaweza kufika ndani ya hifadhi hiyo ukitokea Zambia kupitia Tunduma, ni wastani wa kilometa 170 au Malawi kupitia Wilaya ya Karonga Mkoa wa Mzuzu kwa barabara ni wastani wa kilometa 135.
Kutokea jijini Dar es Salaam kupitia Makambako, Njombe, Makete hadi Kitulo ni wastani wa kilometa 963 na kutoka Dar es Salaam, Chimala, Matamba hadi Kitulo ni wastani wa kilometa 836.
Huduma za hoteli na malazi zinapatikana kwa urahisi katika Jiji la Mbeya ambako kuna hoteli kadhaa zenye hadhi ya kitalii. Pia katika mji wa Matamba ambao upo jirani na hifadhi hii, kuna nyumba za wageni.
Hata hivyo, kutokuwapo kwa juhudi za kutosha katika kuhamasisha wananchi kutembelea hifadhi hiyo kumechangia vivutio vingi vya utalii kutofahamika hata kwa baadhi ya wenyeji.
Uchunguzi umebaini kuwa licha ya Mkoa wa Njombe kuwa na vivutio adimu vya utalii, ikiwamo Hifadhi hiyo ya Kitulo bado wakazi wake hawana mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo, hali ambayo inachangia kutofahamika kwa vivutio hivyo.
Wananchi walio wengi wanadhani wanaostahili kutembelea vivutio hivyo ni watalii kutoka nje ya nchi pekee. Pia baadhi yao hawajui vivutio vya utalii vilivyopo Njombe wakiamini kuwa fursa ya utalii ipo katika mikoa ya Kaskazini pekee na siyo Kusini.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Allan Kijazi akizungumzia hifadhi za taifa kwa ujumla anasema hadi sasa shirika lake linasimamia hifadhi 16 za taifa ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukuza pato la taifa.
Kijazi amezitaja changamoto zinazozikabili hifadhi za taifa kuwa ni pamoja na ujangili unaotokana na biashara za kujikimu, upungufu wa maji katika baadhi ya hifadhi wakati wa kiangazi, migogoro ya mipaka katika baadhi ya hifadhi na mwingiliano kati ya wanyamapori na binadamu.



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

2 comments:

  1. Haya ni maajabu lakini sisi wenyewe bado tupo ktk usingizi mzito,mimi naona tatizo lipo kwa hawa ndugu zetu wa wizara ya utalii kwa kuwa bado hawajitangazi na pia sisi wenyewe hatuna mwamko wa kutembelea hifadhi zetu.la wajibu sasa wizara inatakiwa ijitangaza na pia kuzitangaza mbuga zetu zote kwa ndani ya nchi na nje ya nchi.Tumepewa neema nyingi na Mungu lakini tunashindwa kuzitumia hebu tujitafakari

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ahsante ndg kiona Mbali kwa ujumbe wako. Nimatumaini yangu wausika wameiona. Ahsante kwa kupaza sauti.endelea kutembelea edusportstz kwa habari nyingine zaidi

      Delete

Edusportstz