YANGA, COASTAL ZATINGA NUSU FAINALI CRDB FEDERATION CUP

YANGA ikiwa kwenye ubora wa hali ya juu  imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa mara ya tano mfululizo baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 2-0 kwenye mchezo mkali uliopigwa katika Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni.

Awali ulikuwa unatajwa kuwa mchezo mgumu kwa Yanga kutokana na historia ya uwanja huo ambao timu hiyo ilikuwa haijawahi kupata ushindi wowote hapo, lakini vijana hao wa Jangwani walionyesha kiwango cha juu na kutawala kwenye vipindi vyote viwili vya mchezo huo.

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza Yanga inacheza baada ya hivi karibuni kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji ilipolala kwa mabao 3-2, ikiwa ni mara ya kwanza timu hiyo inapoteza mchezo wa ligi msimu huu.

Kwenye kikosi cha Yanga kilichoanza, kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha hivi karibuni beki na nahodha wa timu hiyo Bakari Mwamnyeto alikosekana hata kwenye benchi la timu hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Frank Assinki, ambaye alionyesha kiwango kizuri.

Wakianza kwa kasi kwenye mchezo huo, JKT walianza kwa kuizawadia Yanga bao baada ya beki wa timu hiyo Hassan Wahabi kujifunga katika dakika ya 33 wakati akiokoa krosi ya beki Chadrack Boka.

Baada ya bao hilo, Yanga iliendelea kuonyesha kiwango cha juu ambapo ilifanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Mudathir Yahaya katika dakika ya 39 ya mchezo, akimfunga kirahisi kipa Ramadhan Chalamanda, baada ya kuiwahi pasi ya Pacome Zouzoua.

Mabao hayo mawili yaliifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele huku pia ikionyesha kucheza vizuri dakika hizo 45 za kwanza.

Kipindi cha pili, Yanga ikiendelea kutengeneza nafasi kupitia Dube,Okello na Boka lakini ikapoteza umakini kidogo kwenye kuzitumia na mchezo huo kumalizika kwa ushindi wa 2-0.

Hii ni mara ya pili Yanga inaitupa nje JKT kwenye michuano hiyo baada ya msimu uliopita kuichapa mabao 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainali. Yanga sasa inasubiri mshindi  kati ya Mashujaa na Azam zinazocheza leo jioni.

Katika mchezo wa mapema uliopigwa, Coastal Union ilifanikiwa kwenda nusu fainali baada ya kuichapa Singida BS kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkakwani Tanga kumalizika dakika 90 kwa suluhu, sasa timu hiyo inasubiri mshindi kati ya Simba na TRA mechi itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa KMC Complex.

The post YANGA, COASTAL ZATINGA NUSU FAINALI CRDB FEDERATION CUP appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/z0TOAJt
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post