WAKATI Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) ikitarajia kuanza kesho kwenye Uwanja wa Don Bosco, Upanga, baadhi ya makocha wamesema timu zilizofanya usajili mkubwa zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu, huku uzoefu ukipewa nafasi kwa baadhi ya timu kongwe.
Kocha kutoka Temeke, Ally Issa alisema usajili mkubwa uliofanywa na timu mbalimbali umechagizwa na bonasi zitakazotolewa na wadhamini kwa timu zitakazoshinda ligi hiyo.
“Kwa kweli kila timu inataka bonasi hiyo, ndiyo maana imeamua kufanya usajili mkubwa. Huku baadhi ya timu zikishindwa kufanya hivyo kutokana na kukosa wadhamini wa kuzisaidia,” alisema Issa.
Kwa upande wa wanaume, timu 16 zitashiriki ligi hiyo huku Dar City, Stein Warriors, DB Oratory, Mlimani BC, UDSM Outsiders na Pazi zikionekana kufanya usajili mkubwa zaidi kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.
ZILIVYOSAJILI
Bingwa mtetezi Dar City imeboresha kikosi chake kwa kuwasajili nyota wanne kutoka Stein Warriors ambao ni Sisco Ngaiza, Jonas Mushi, Felix Luhamba na Evans Davies. Wengine ni Fotius Ngaiza kutoka Vijana “City Bulls” na Ethan Billy kutoka Pazi, huku wachezaji wa kimataifa ni Shalom Ikedigwe (Nigeria), Elijah Mukelabai (Zambia), Cheikh Bamba Diallo (Senegal) na Nkosinathi Sibanyoni (Afrika Kusini).
Stein Warriors imewasajili Jimmy Brown kutoka JKT pamoja na Swalehe Burhan, Ally Mohamed na Adam Kassimu kutoka Dar City. Wachezaji wa kimataifa waliotua katika kikosi hicho ni Moise Bukengu kutoka DR Congo na Spoican Ngoma kutoka Zambia.
DB Oratory nayo imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota wa kimataifa Yang Ogweno kutoka Kenya, Chad Kampema na Oswald Bera kutoka DR Congo pamoja na Ayom Ayor kutoka Sudan Kusini.
Vijana “City Bulls” imemsajili Mopele Baraka kutoka JKT, Dominic Dogan kutoka DB Oratory na Rahim Ramadhani kutoka KIUT, huku nyota wa kimataifa ni Philip Otieno (Kenya), Nathan Kangudi (DR Congo) na Soro Godfrey (Uganda).
Mlimani BC iliyopanda daraja msimu huu imeboresha kikosi chake kwa kuwasajili nyota wa kimataifa David Buyamba, Jeancy Traore na Henock Kakumba wote kutoka DR Congo.
UDSM Outsiders imewasajili Alfani Mustafa kutoka JKT pamoja na Iverson Mgunda kutoka Vijana “City Bulls”, huku wachezaji wa kimataifa waliotua kambini hapo ni Felix Muteba, Celly Ntambwe na Manu Mwamba wote kutoka DR Congo.
Timu kongwe ya Pazi nayo imeboresha kikosi chake kwa kumsajili Erick Lugora kutoka Dar City, huku kwa upande wa nyota wa kimataifa ikipewa nguvu na Robert Tasire kutoka Kenya, Lerry-Rostand kutoka Gabon pamoja na Yannick Kaboy na Joao Kasungwa kutoka DR Congo.
Hata hivyo,JKT, ABC na Savio zinaonekana kuamini zaidi uzoefu na ukongwe baada ya kutofanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya kuelekea msimu huu wa BDL.
Kwa upande wa Veins BC na Ukonga Kings, zimeonekana kuongoza kwa kusajili idadi kubwa ya wachezaji wazawa. Veins BC imewasajili Ronaldo Kisobwe, Baraka Sadiki na Jordan Manangi kutoka JKT huku Ukonga Kings ikiendelea kuwaamini wachezaji walioipandisha daraja kucheza BDL msimu huu.
Wakati huo huo, Srelio, Magone na Mchenga BC zimepewa kazi ya kujipanga vizuri kama zinataka kutoa ushindani mkubwa kutokana na kutofanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya.
TUKUTANE KESHO
Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza kesho Jumamosi, Ukonga Queens itacheza dhidi ya Mgulani Queens, City Queens dhidi ya Kurasini Divas na UDSM Queens dhidi ya Pazi Queens. Michezo mingine ni Chui dhidi ya Srelio, Twalipo Queens dhidi ya Polisi Stars, Mchenga BC dhidi ya Magone BC, DB Troncatti dhidi ya Jeshi Stars pamoja na Savio dhidi ya Vijana.
Akizungumzia usinduzi wa ligi hiyo, Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa BDL alisema utafanyika Jumapili katika mechi kati ya Stein Warriors na JKT.
VITA IKO HAPA
Kabla ya mechi hiyo, Ukonga Kings itacheza dhidi ya Mlimani BC huku Tausi Royals ikitarajiwa kuvaana na Vijana Queens katika mechi ya wanawake inaotabiriwa kuwa mkali kutokana na usajili mzuri uliofanywa na timu zote mbili.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana mwaka jana, Vijana ilishinda pointi 65-50.
Tausi Royals inayofundishwa na Daudi Maiga pamoja na Mourine Sinza imeboresha kikosi chake kwa kuwasajili Noela Renatus kutoka JKT, Judith Edward kutoka Arusha na Grace Innocent kutoka JKT. Kwa upande wa nyota wa kimataifa, timu hiyo imewasajili Divine Irakoze na Asliyah Havyarimana kutoka Burundi.
Wachezaji waliokuwapo katika kikosi hicho msimu uliopita ni Tumaini Ndossi, Tumwagile Mwaipola, Jacline Muzuka, Diana Mwedi, Lissa Masanja, Naserian Mollel, Mahewa Allan, Lucy Masele, Ramla Mohamed, Asumpta Kamanda, Khadija Saidi, Keita Menda na Juliana Mashaka.
Kwa upande wa Vijana imemsajili Maria Mbena kutoka Pazi Queens pamoja na nyota wa kimataifa Aurelia Irebu kutoka DR Congo, Natalie Akinyi kutoka Kenya na Lisiane Ngomba kutoka DR Congo ambao wataungana na nyota wazawa waliocheza msimu uliopita akiwemo Imelda Hango, Roselny Israel, Frida Zabloni, Nasra Irebu na Rahabu Sebastian.
The post USAJILI WA KIBABE KUNOGESHA LIGI YA KIKAPU DAR BDL appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/NPs8hE2
via IFTTT
Post a Comment