NI zamu ya mabinti, baada ya mechi ya watani wa jadi ya kaka zao Simba na Yanga iliyotoka kwa sare ya 2-2, sasa ni zamu ya Simba Queens ikiikaribisha Yanga Princess Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam leo kuanzia saa 11 jioni.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza Yanga ikiwa mwenyeji ilichapwa mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na washambuliaji Jentrix Shikangwa na Aisha Mnunka.
Huo ni mzunguko wa 16 wa ligi ya Wanawake na mechi ya leo inatarajiwa kuwa na msisimko na ushindani wa aina yake.
Ni dabi ya heshima, historia, mbinu za makocha na ushindani wa kuwania pointi unaoweza kubadilisha msimamo wa ligi kwenye nafasi za juu.
DABI YA UBINGWA
Simba Queens inaingia katika mchezo huo ikiwa kileleni katika msimamo wa ligi kwa pointi 43 baada ya kucheza mechi 15. Katika mechi hizo, Simba imeshinda mechi 14 na kutoka sare moja, rekodi inayodhihirisha uimara wao mkubwa msimu huu.
Hadi sasa Simba Queens pekee ndio haijapoteza mechi ikiweka rekodi ya aina yake na ndiyo timu pekee iliyoruhusu mabao machache ikifungwa mawili.
Yanga Princess wao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 39 kwa idadi hiyo hiyo ya michezo. Hiyo ina maana kwamba tofauti kati ya timu hizo mbili ni pointi nne pekee.
Iwapo Simba Queens itashinda, itafikisha pointi 46 na kuacha pengo la pointi saba dhidi ya Yanga Princess. Hali hiyo itawapa nafasi kubwa zaidi ya kuusogelea ubingwa, hasa kwa kuzingatia ligi inaelekea ukingoni.
Lakini kama Yanga Princess itashinda, itafikisha pointi 42 na kupunguza tofauti hadi pointi moja tu. Matokeo hayo yatafufua upya mbio za ubingwa na kuongeza presha kubwa kwa Simba Queens katika mechi sita zilizobaki.
Kwa mantiki hiyo, mechi hii inaweza kutafsiriwa kama fainali ndogo ya msimu.
Hata hivyo, Simba ikishinda itahitaji kushinda mechi nne mfululizo kati ya sita zilizosalia ili kutangazwa mabingwa kabla ya ligi kutamatika.
VITA YA NAFASI YA PILI
Mbali na mbio za ubingwa, matokeo ya mechi hiyo yanaweza kurejesha vita ya nafasi ya pili. JKT Queens ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38, pointi moja tu nyuma ya Yanga Princess yenye 39.
Iwapo Yanga Princess itapoteza, sio tu itaruhusu Simba Queens kusalia kileleni, bali pia itaipandisha JKT Queens hadi nafasi ya pili.
Hivyo, Yanga inaingia uwanjani ikijua kushindwa kunaweza kuwaacha katika mazingira magumu ya kupoteza nafasi yao.
Kwa Simba, ushindi utakuwa na faida mara mbili kuendelea kujiimarisha kileleni na kuusogelea ubingwa na kudhoofisha mpinzani wao wa jadi.
REKODI ZAO
Tangu mwaka 2019, zimekutana mara 18 kwenye mashindano mbalimbali ikiwemo Ngao ya Jamii, Simba ikiibuka na ushindi mara 12. Yanga ikishinda mara tatu, huku mechi tatu zikitoka sare.
Lakini kwenye ligi timu hizo zimekutana mara 14, Simba ikishinda mara 10, sare mbili na kupoteza mechi mbili huku Yanga ikishinda mechi mbili, sare mbili na kupoteza mbili.
Takwimu hizo zinaonyesha ubabe wa Simba katika miaka ya karibuni, lakini dabi mara nyingi haiangalii takwimu pekee bali mechi hizo huamuliwa na mbinu, ari, nidhamu na uwezo wa kutumia nafasi.
Hata hivyo, upande wa Simba utaingia uwanjani ukiwa na nguvu ya kisaikolojia kutokana na rekodi hiyo nzuri.
VITA YA MAKOCHA
Nje ya mechi hiyo, kutakuwa na pambano la kiufundi kati ya makocha wa timu hizo mbili kwa Edna Lema wa Yanga Princess na Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba Queens.
Edna Lema hataiongoza timu yake akiwa benchi kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyopata katika mechi iliyopita.
Hata hivyo, falsafa yake, maandalizi ya kikosi na maelekezo yake yataendelea kuwa sehemu muhimu ya mpango wa Yanga.
Makocha hawa wawili wanajulikana kwa kusoma vizuri wapinzani wao, kufanya marekebisho ya haraka na kuhimiza nidhamu ya kiufundi.
Dabi hii inaweza kuamuliwa na mabadiliko madogo ya kimkakati, hasa katika eneo la kiungo kwani timu zote mbili zina safu nzuri ya viungo.
VITA YA USHAMBULIAJI
Hadi sasa mshambuliaji wa Yanga, Jeannine Mukandayisenga ndiye kinara wa mabao akiwa na 19, amekuwa nguzo muhimu katika safu ya ushambuliaji ya wananchi.
Kwa uwezo wake wa kujitengenezea nafasi na kumalizia kwa utulivu, ni miongoni mwa washambuliaji tishio kwenye safu ya ulinzi ya Simba.
Kwa upande wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa ni mchezaji wa kutegemewa katika eneo la ushambuliaji akiwa na mabao 12.
Timu zote mbili zina wachezaji wenye uwezo wa kuamua mchezo.
ULINZI
Simba imeonyesha uimara mkubwa kwenye safu ya ulinzi kwa kuruhusu mabao mawili tu katika mechi 15, idadi ndogo ya kuruhusu bao ikionyesha safu yao ya ulinzi ni ngumu kufikika.
Yanga imefunga mabao 44, idadi inayothibitisha uwezo wao mkubwa wa kushambulia hata hivyo imeruhusu mabao 13 ikiwa na wastani wa kuruhusu bao moja kwa kila mechi.
Hivyo, mchezo huu unaleta mlingano wa kuvutia kati ya safu bora ya ulinzi dhidi ya moja ya safu bora zaidi za ushambuliaji.
Dabi ya Simba Queens na Yanga Princess ni zaidi ya mchezo wa kawaida.Ni pambano la heshima, utawala wa soka la wanawake na uthibitisho wa ubora wa kila upande.
Kwa Simba Queens pointi tatu ni muhimu ili kujiweka pazuri kwenye nafasi ya kuwania ubingwa. Kwa Yanga Princess, ushindi utakuwa na maana kwamba mbio za ubingwa bado ziko wazi.
WASIKIE WENYEWE
Akizungumzia mechi hiyo mshambuliaji wa Simba, Aisha Mnunka anasema mechi hiyo kama wakishinda inaenda kuwapa nafasi nzuri ya kunyakua taji.
“Ni mechi kubwa kila mmoja amejiandaa kwa namna yake sisi tumejiandaa vizuri kwa ajili ya pointi tatu laakni siwezi kumzungumzia zaidi mpinzani yote kwa yote itaenda kujulikana nani mshindi na itaenda kutupa tasiwira nzuri,” anasema Mnunka
Kiungo wa Yanga, Agnes Pallangyo anasema anaamini mechi ya dabi haiamuliwi na mbinu pekee za makocha bali pia na kujitoa kwa wachezaji kwa asilimia 100.
“Naamini kila mchezaji ana morali na anatamani kushinda mechi kwa sababu ni mechi ya maamuzi, mbinu pekee hazitoshi kwa sababu muda mwingine inaweza kukubalia au kukataa ikikataa jitihada zetu zitaamua.”
The post DABI YA KISASI NA MABINGWA WPL appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/lXRfS4r
via IFTTT
Post a Comment