SHIRIKISHO la Soka Ulaya (UEFA), limetoa ufafanuzi kuhusu tukio la utata lililopelekea Arsenal kunyimwa penalti katika mechi ya nusu fainali ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid.
Tukio hilo lilitokea katika dakika ya 78 ya mchezo wakati mchezaji Eberechi Eze, aliyeingia akitokea benchi, alipoanguka ndani ya eneo la hatari baada ya kukumbana na beki wa Atletico, David Hancko.
Awali, mwamuzi wa kati Danny Makkelie alionekana kuashiria kuwa ni madhambi na kuipa Arsenal penalti. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa mguso kati ya mguu wa Hancko na Eze, mwamuzi wa video (VAR) aliingilia kati na kumtaka Makkelie kwenda kutazama marudio kwenye VAR.
Baada ya kutazama marudio hayo mara kadhaa, Makkelie alibatilisha uamuzi wake wa awali na kuamuru mechi iendelee, jambo ambalo liliwanyima Arsenal nafasi ya kupata bao la pili.
Uamuzi huo ulimwacha meneja wa Arsenal, Mikel Arteta, akiwa na hasira, huku akikosoa hatua hiyo kwa kusema: “Haikubaliki kabisa. Ni uamuzi ambao haueleweki kwenye hatua kama hii ya mashindano.”
Katika taarifa fupi ya kufafanua msimamo wao, UEFA imetetea uamuzi wa mwamuzi kwa kusema kuwa hakukuwa na uvunjifu wa sheria uliotokea.
“Mchezaji wa Atletico, namba 17 (Hancko), hakufanya madhambi dhidi ya mpinzani wake,” inasomeka taarifa hiyo ya UEFA.
Ufafanuzi huu unakuja huku kukiwa na mijadala mikali miongoni mwa wachambuzi na mashabiki wa soka kuhusu matumizi ya VAR kwenye mechi kubwa, huku Arsenal sasa ikilazimika kupambana kwenye mechi ya mkondo wa pili itakayopigwa jijini London, England ili kufuzu fainali.
The post UEFA YAFAFANUA SABABU YA ARSENAL KUNYIMWA PENALTI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/Mg1E7qx
via IFTTT
Post a Comment