MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union ni miongoni mwa mechi ngumu kwa kikosi hicho
Amerejea kumbukumbu ya msimu uliopita ambapo wapinzani hao walichangia kuinyima Simba nafasi ya kufikia malengo yake ya ubingwa.
Ahmed amesema sare ya mabao 2-2 waliyopata dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa KMC iliigharimu Simba kwa kupoteza alama mbili muhimu katika mbio za ubingwa, jambo lililowaacha na maumivu makubwa.
Kutokana na historia hiyo, amesema kikosi cha Simba kinaingia katika mchezo huo kikiwa na kumbukumbu ya matokeo hayo, hali inayowapa hamasa ya kupambana kwa nguvu zaidi safari hii ili kuepuka makosa yaliyopita.
“Mechi dhidi ya Coastal Union ni ngumu kwa sababu ni miongoni mwa timu zilizochangia kutunyima ubingwa msimu uliopita,” amesema Ahmed Ally.
Ameongeza kuwa maandalizi ya timu yamekuwa mazuri, yakilenga kurekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza hapo awali ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika mchezo huo muhimu.
Kwa mujibu wa Ahmed, licha ya Coastal Union ya msimu huu kuonyesha ushindani mkubwa na kuwa tofauti na ile ya msimu uliopita, Simba nayo ipo katika kiwango kizuri na tayari kwa pambano hilo.
“Tunaingia uwanjani tukiwa na kumbukumbu ya maumivu ya nyuma, lakini safari hii tumejipanga vizuri. Tunatambua ubora wa wapinzani wetu, lakini nasi tuko tayari kuhakikisha tunapata pointi tatu,” amesema.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho kuikabili Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Jenerali Isamuhyo, ikiwa na lengo la kuondoka na ushindi ili kujiimarisha zaidi kwenye mbio za ubingwa.
The post SIMBA YAKUMBUKA MAUMIVU, YAIVAA COASTAL KWA HASIRA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/SHLIqv6
via IFTTT
Post a Comment