BAJABER AWAREJESHA SIMBA TABASAMU, BARKER AWEKA MIPANGO

KIUNGO  wa Simba, Mohammed Bajaber, ameanza kurejea taratibu kwenye ubora wake baada ya kupata nafasi ya kucheza dakika 45 ambazo zimeonyesha mwanga kwa benchi la ufundi, huku kocha Steve Barker akifichua mipango yake juu ya staa huyo.

Mara ya mwisho Bajaber kuonekana uwanjani ilikuwa Januari 10, 2026, alipocheza kwa dakika tisa tu katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, alilazimika kutoka mapema baada ya kukaa chini mwenyewe akishika mguu wake wa kushoto nyuma ya paja, akionekana kuumia.

Alitolewa dakika ya 11 na nafasi yake kuchukuliwa na Kibu Denis, katika mchezo ambao pia ulikuwa wa kwanza kwa kocha Steve Barker kuiongoza Simba kwenye ligi tangu aanze kazi yake.

Hata hivyo, katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Mafunzo uliochezwa juzi, Bajaber alirejea kwa kupewa dakika 45 za kipindi cha pili, akiingia kuchukua nafasi ya kinda Ladack Chasambi. Aliingia sambamba na mshambuliaji Seleman Mwalimu ambaye ndiye aliyefunga bao la ushindi kwa Simba.

Ndani ya dakika hizo 45, Bajaber alionyesha kiwango cha kuvutia, akipiga pasi 36 ambapo 35 zilifika kwa usahihi mkubwa. Pia alipiga krosi moja kutoka upande wa kushoto iliyokosa mlengwa na kufanikiwa kupokonya mpira mara moja.

Mbali na hilo, kiungo huyo alionyesha kupambana kwa nguvu katika matukio matatu, akifanikiwa mara mbili kulinda mpira. Ingawa hakutengeneza nafasi nyingi za wazi za kufunga, alionekana kurejesha hali yake ya kujiamini tofauti na mechi zake za awali alipokuwa na hofu ya kuumia tena.

Bajaber, ambaye hadi sasa ana bao moja kwenye ligi kabla ya kukumbwa na majeraha yaliyomuweka nje ya kikosi kwa muda, anaonekana kurejea kwa kasi huku akijenga upya kiwango chake.

Barker amesema  amefurahishwa na kiwango alichoonyesha Bajaber, akisisitiza kuwa bado anahitaji kurejeshwa taratibu ili kufikia ubora wake wa juu.

Barker ameongeza kuwa anatamani kumtumia zaidi kiungo huyo kwenye mechi za ligi, akieleza kuwa uwepo wake uwanjani huleta hofu kwa wapinzani huku ukizua furaha kubwa kwa mashabiki wa Simba.

The post BAJABER AWAREJESHA SIMBA TABASAMU, BARKER AWEKA MIPANGO appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/6TruKXI
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post