KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, ameweka wazi msimamo wa kikosi chake baada ya kumaliza nusu ya kwanza ya msimu wakiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akisisitiza kuwa hawana mpango wa kuachia nafasi hiyo kirahisi.
Kauli hiyo inakuja licha ya matokeo yasiyoridhisha katika michezo yao miwili ya hivi karibuni, Yanga ilidondosha alama nne na kuwapa nafasi wapinzani wao Simba kusogea kwa kasi, wakipunguza pengo la pointi kutoka tano hadi moja.
Hali hiyo imeibua wasiwasi kwa baadhi ya mashabiki, wakihofia timu hiyo inaweza kuanza kuyumba katika mbio za ubingwa.
Pedro ameondoa hofu hiyo kwa kusisitiza kuwa mafanikio ya Yanga hayajatokana na bahati, bali ni matokeo ya juhudi kubwa, nidhamu na mshikamano wa hali ya juu ndani ya kikosi.
Kocha huyo ameifananisha timu yake na chuma kigumu, ameeleza kuwa uimara wao si rahisi kuvunjika, hasa katika kipindi hiki muhimu cha msimu.
Amesisitiza kuwa moja ya silaha kubwa waliyonayo ni moyo wa kupambana, ambao wachezaji wake wameuonyesha mara kwa mara wanapokutana na changamoto ndani na nje ya uwanja.
Pedro amekumbusha namna walivyoanza msimu kwa kusuasua na kujikuta nyuma ya wapinzani wao katika michezo ya awali, lakini kupitia mshikamano na kujituma waliweza kubadili mwelekeo na kupanda hadi kileleni jambo analoliona kama uthibitisho wa ubora wao.
“Nafasi tiliyonayo kwa sasa ni halali na tumeipata kwa jasho lao letu, hatupo tayari kuiachia. lengo letu ni kuendelea kubaki kileleni hadi mwisho wa msimu na hatimaye kutwaa ubingwa,” amesema.
Pedro pia amepongeza ari na kujituma kwa wachezaji wake, akibainisha kuwa kikosi hicho kina kiu kubwa ya mafanikio na hakiko tayari kukata tamaa.
Ameongeza kuwa tayari wameanza maandalizi ya mechi zijazo, wakilenga kuendeleza ubora wao na kulinda nafasi yao ya juu.
The post SIRI NI CHUMA, HATUTOKI KILELENI, KOCHA YANGA AITAMBIA SIMBA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/zwo6yPg
via IFTTT
Post a Comment