IBENGE AZIKOMALIA SIMBA NA YANGA VITA MPYA LIGI KUU

KOCHA Mkuu wa Azam, Florent Ibenge, amesema licha ya matokeo mazuri waliyonayo lakini hafurahii sana kwani pointi walizozidiwa na Yanga na Simba zinampa uchungu kufikia malengo yao ya ubingwa msimu huu.

Amesema kutokana na hali hiyo, anaendelea kuwaandaa vyema nyota wake kuhakikisha kila mchezo ulio mbele yao wanapata ushindi, huku akiivimbia Tanzania Prisons kuhakikisha wanachukua pointi tatu kesho jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine.

Azam iliyopo nafasi ya tano kwa pointi 23, imezidiwa moja na Simba iliyopo nafasi ya tatu na pointi sita dhidi ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga na kufanya vita ya ubingwa msimu huu kuwa nzito wakati timu hizo zikiwa bado hazijamaliza duru la kwanza.

Akizungumza jijini hapa, Ibenge amesema matokeo waliyonayo si mabaya sana japokuwa hayajamfurahisha sana kutokana na kuzidiwa pointi na Simba na Yanga, hali inayomfanya kupambana kuwashusha wakongwe hao.

Amesema timu hiyo inayo mikakati yake akieleza kuwa kinachompa matumaini zaidi ni namna nyota wake wanavyopambana ndani ya uwanja kusaka ushindi akieleza kiwango wanachoonesha kinampa nguvu.

“Kikubwa ni kupambana kuondoa pengo lililopo la pointi dhidi yetu, Simba na Yanga, tunao mkakati wetu msimu huu katika kufanya vizuri na vijana wanapambana na wanaonesha soka safi,” amesema Ibenge.

Kuhusu mechi ya kesho dhidi ya Tanzania Prisons, amekiri kutokuwa nyepesi akieleza watakuwa makini akibainisha kutokuwapo kwa baadhi ya wachezaji akiwamo Feisal Salum haitakuwa tatizo kwani anacho kikosi bora.

Kwa upande wake nahodha wa Azam, Lusajo Mwaikenda, amesema mechi hiyo itakuwa mgumu kutokana na wapinzani nafasi waliyopo akieleza kuwa hawataki yawakute yaliyowatokea Liverpool mbele ya Wolves walipolala 2-1.

“Bado tuna ubora kwenye Ligi Kuu licha ya ratiba ngumu mfululizo, tunajua ugumu wa mchezo dhidi ya Prisons waliopo chini kwenye msimamo, kila mmoja aliona kilichowakuta Liverpool dhidi ya Wolves,” amesema Mwaikenda.

The post IBENGE AZIKOMALIA SIMBA NA YANGA VITA MPYA LIGI KUU appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/CBsW3Xf
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post