CHAMA, OURA HATIANI MEJA JENERALI ISAMUHYO

KIKOSI cha B19 maarufu kama Mabeberu wa Jiji kimeweka wazi kuwa kitaingia uwanjani kwa kujiamini bila hofu mbele ya mabingwa wa jadi, Simba SC.

Timu hiyo imesisitiza kuwa imeandaa mpango kazi maalum wa kuwadhibiti nyota hatari wa Simba, Clatous Chama na Anicet Oura.

Kocha Mkuu wa B19, Behi Mbaya, amesema pamoja na kuwaheshimu Simba kama timu kubwa yenye uzoefu na ubora,  ameifanyia uchambuzi wa kina na kubaini maeneo wanayoweza kuyatumia kuwabana wapinzani wao.

Ameeleza kuwa maandalizi yao yamelenga zaidi kuwazuia viungo hao washambuliaji wasiendeshe mchezo wao wa kawaida.

Kwa mujibu wa Behi, wanafahamu hatari ya Chama na Oura wanapocheza katikati ya uwanja wakitengeneza mashambulizi ya kushtukiza.

Hivyo, mkakati wao ni kuwabana kwa ukaribu, kuwanyima nafasi ya kupokea na kusambaza mipira, pamoja na kulazimisha mashambulizi ya Simba yapitie pembeni ambako wanaamini wataweza kudhibiti hatari hiyo.

Mchezo huo wa hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB unatarajiwa kupigwa Jumamosi, Machi 5, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Behi amesema morali ya kikosi chake ipo juu na wachezaji wanaelewa uzito wa pambano hilo.

“Maandalizi yanaendelea vizuri. Tunawaheshimu Simba kwa sababu ni timu kubwa, lakini tumeona wanavyocheza na tunajua ni wakati gani wanakuwa hatari zaidi,” amesema Behi, akiongeza kuwa ushindani utakuwa mkubwa kwa kuwa kila timu inahitaji ushindi.

B19 kwa sasa inashiriki Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya 13, lakini imeonyesha makali yake katika michuano ya kombe hili baada ya kuvuka hatua iliyopita kwa ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Dhujau kutoka Katavi.

Ushindi huo umeongeza ari na kujiamini kwa Mabeberu wa Jiji kuelekea pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa.

The post CHAMA, OURA HATIANI MEJA JENERALI ISAMUHYO appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/FAKzPnE
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post