CHAMAZI KIZANI, YANGA WAKUMBUKA MAUMIVU YA 2024

WAKATI Serikali ikiendelea na maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 na kuufungua rasmi Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa shughuli hizo, uongozi wa Azam FC umechukua maamuzi mazito kwa kuhamishia mchezo wao dhidi ya Yanga kwenye dimba la nyumbani la Azam Complex Stadium, Chamazi.

Awali, dabi hiyo ya Dar es Salaam ilipangwa kuchezwa Machi 15, 2026 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hata hivyo, baada ya ratiba kubadilika kutokana na maandalizi ya AFCON, Azam wameamua kutumia uwanja wao wa nyumbani, hatua inayotafsiriwa na wengi kama kuwapeleka wapinzani wao kwenye mazingira magumu zaidi.

Kwa mujibu wa Meneja wa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabiti maarufu kama ‘Zaka za Kazi’, kuanzia sasa michezo yote mikubwa ambayo wao ni wenyeji itachezwa Azam Complex isipokuwa ile ya michuano ya kimataifa.

Amesisitiza kuwa dabi ya Mzizima dhidi ya Simba pamoja na ile ya Dar es Salaam dhidi ya Yanga zitapigwa Chamazi.

Kauli hiyo imeamsha kumbukumbu kwa mashabiki wengi, hasa ukizingatia historia ya hivi karibuni ya Yanga katika dimba hilo. Mwaka 2024, Yanga waliwahi kuutumia Azam Complex kama uwanja wao wa nyumbani, lakini mambo hayakuwa rahisi.

Walipoteza michezo miwili mfululizo, wakifungwa 1-0 na Azam FC Novemba 2 na 8, kabla ya kuangukia tena kwa kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Tabora United.

Katika mchezo huo dhidi ya Tabora United, mabao yalifungwa na Offen Chikola pamoja na Nelson Munganga, matokeo yaliyozidi kuibua mjadala kuhusu uimara wa Yanga wanapocheza Chamazi. Baada ya kupoteza alama sita muhimu, Yanga walilazimika kubadili uwanja na kuhamishia mechi zao katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.

Sasa, kurejea kwa Yanga Azam Complex kunatajwa kama mtihani mwingine mgumu. Azam wakiwa nyumbani na wakijiamini, huku Yanga wakikumbukwa kwa kumbukumbu zisizo nzuri katika dimba hilo, dabi hii ina kila dalili ya kuwa na presha, ushindani na hisia kali kwa pande zote mbili.

Yanga watafuta makosa ya zamani na kuvunja mwiko wa Chamazi, au Azam wataendelea kuifanya Azam Complex kuwa machinjio kwa watani wao.

The post CHAMAZI KIZANI, YANGA WAKUMBUKA MAUMIVU YA 2024 appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/7j2VlBD
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post