Kipa wa Yanga, Djigui Diarra amepewa adhabu ya kufungiwa mechi tatu na adhabu ya faini ya Sh4 milioni kutokana na makosa mawili tofauti ya utovu wa nidhamu aliyofanya katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Kwa mujibu wa adhabu zilizotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi zilizotangazwa leo, Ijumaa, Machi 27, 2026, Diarra ametozwa faini ya Sh2 milioni na kifungo cha mechi tatu kwa kosa la kumshambulia Refa wa mchezo huo.
Diarra pia ametozwa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la kuonyesha ishara ya matusi mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Kipa huyo amepewa adhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi Kuu ambayo inafafanua kwamba mchezaji yeyote atakayekutwa na hatia ya kosa la kumshambulia mwamuzi, kiongozi, mtazamaji au mtu yoyote kwa namna yoyote ile, iwe kwa matusi au kwa vitendo, atapewa adhabu ya kufungiwa michezo isiyopungua mitatu na/au faini isiyopungua Sh500,000 mpaka Sh2 milioni.
Refa wa mchezo baina ya Yanga na Mtibwa Sugar, Gilbert Mrina wa Kilimanjaro, ameshushwa daraja kwa kosa la kushindwa kumchukulia hatua Djigui Diarra kwa utovu wa nidhamu alioonyesha katika mchezo huo.
Refa msaidizi Abdulaziz Ally wa Arusha, amefungiwa mizunguko mitano kwa kosa la kushindwa sheria ya kuotea.
Wakati huohuo, Simba imetozwa faini ya Sh10 milioni kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa za maji marefa wa mchezo baina ya timu yao na Pamba Jiji.
Adhabu nyingine imeenda kwa TRA United ambayo imetozwa Sh500,000 kwa kosa la wachezaji wake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mchezo dhidi ya Yanga.
The post DIARRA MNJE MECHI TATU, AMPONZA MWAMUZI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/47CTkQU
via IFTTT
Post a Comment