MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa licha ya kiungo mshambuliaji Elie Mpanzu kutokuwa na muendelezo mzuri kwa sasa, bado klabu hiyo ina imani kubwa na mchango wake wa baadaye ndani ya kikosi hicho.
Ahmed amesema uongozi wa Simba unatambua uwezo mkubwa wa Mpanzu, jambo lililowasukuma kumuongezea mkataba ili kuendelea kubaki ndani ya timu hiyo.
Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha hawapati changamoto ya kutafuta mbadala wa kiwango kama chake siku zijazo.
Amebainisha kuwa wakati mkataba wa mchezaji huyo ulikuwa unakaribia kufikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu, kulikuwa na vilabu vingi vilivyokuwa vinahitaji huduma yake, ndani na nje ya Tanzania, hali iliyoongeza umuhimu wa kumbakiza.
“Tunatambua ubora wake. Ni kweli amepitia changamoto za hapa na pale, lakini tunaamini ana uwezo mkubwa wa kuisaidia Simba kwa miaka ijayo. Hatukutaka kumuacha halafu baadaye tukaanza kupata tabu ya kutafuta mchezaji wa aina yake,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa hata kama wangeamua kuingia sokoni kufanya usajili wa mbadala, bado haikuwa rahisi kupata mchezaji mwenye ubora unaofanana na wake, akisisitiza kuwa mara nyingi usajili huwa ni wa kubahatisha.
Kuhusu tetesi za dau la usajili wa Mpanzu linalodaiwa kufikia Shilingi bilioni moja, Ahmed amesema hana uhakika nalo, akieleza kuwa masuala ya kimkataba ni siri kati ya mchezaji na mwajiri wake.
The post BILIONI MOJA YA MPANZU YAZUA MJADALA, SIMBA YATOA KAULI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/aAcjg6T
via IFTTT
Post a Comment