DURU la kwanza wa Ligi ya Championship, unahitimishwa rasmi wikiendi hii na baada ya jana kuchezwa mechi mbili, nyingine tatu zitachezwa leo Jumamosi na kesho Jumapili, huku vita kali ya kuwania kupanda daraja ikiwa ni kwa timu zilizopo nafasi nne za juu.
Barberian zamani Kiluvya United iliyoifunga TMA ya jijini Arusha mabao 2-1, wiki iliyopita ikiwa ni ushindi wa kwanza kwa kikosi hicho tangu msimu huu umeanza, itacheza dhidi ya Songea United iliyotoka suluhu (0-0) na Hausung ya Njombe.
Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Kituo cha TFF Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Barberian inaingia ikiwa inaburuza mkiani na pointi saba, baada ya kikosi hicho kushinda mmoja tu, kikitoka sare minne na kupoteza tisa kati ya 14, iliyocheza.Maafande wa Polisi Tanzania baada ya kuchapwa mabao 4-2, dhidi ya Mbeya Kwanza, inarejea kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi kuikaribisha Gunners ya Dodoma, ambayo mechi ya mwisho ilishindwa kutamba na kuchapwa nyumbani na Kagera Sugar 3-0.
Mechi ya mwisho leo Jumamosi, itapigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora na Mbeya Kwanza iliyoichapa Polisi Tanzania mabao 4-2, itacheza dhidi ya Kagera Sugar, yenye morali pia baada ya kuichapa Gunners kutoka jijini Dodoma 3-0.
Raundi ya 15, itahitimishwa kesho Jumapili kwa mechi tatu kupigwa, ambapo Stand United ‘Chama la Wana’, iliyochapwa bao 1-0, dhidi ya Geita Gold, itaikaribisha African Sports ya mjini Tanga, yenye kumbukumbu ya kufungana bao 1-1 na Bigman.
Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mbuni iliyoichapa Transit Camp mabao 3-0, itabakia uwanjani hapo kwa kuikaribisha B19, inayoingia katika mechi hiyo na morali baada ya wiki iliyopita kuifunga KenGold ya jijini Mbeya 2-1.
Mechi ya mwisho kesho Jumapili itapigwa kwenye Uwanja wa Amani uliopo Halmashauri ya mji wa makambako katika Mkoa wa Njombe na Hausung iliyotoka suluhu (0-0) dhidi ya Songea United, itaikaribisha TMA iliyochapwa 2-1 na Barberian.Kocha wa Barberian, Kheri Mohamed, amesema baada ya timu hiyo kushinda mechi ya kwanza msimu huu, anaamini wachezaji kwa sasa watakuwa na morali zaidi, licha ya kukiri mwanzo mgumu kutokana na kukosa uzoefu kwa nyota wengi wa kikosi hicho.”Ni kweli msimu huu umekuwa ni mgumu sana kwetu tofauti na matarajio, ila bado tutaendelea kupambana hasa katika raundi hii ya pili, kikubwa kwa sasa ni kuhakikisha hatudondoshi pointi zaidi kama tulivyofanya hapo mwanzoni,” amesema Kheri.
The post VITA YA KUPANDA LIGI KUU YAPAMBA MOTO appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/kDQyo0H
via IFTTT
Post a Comment