WAKATI uongozi wa klabu ya Simba SC ukikamilisha taratibu zote za vibali na leseni kwa wachezaji wapya waliowasajili dirisha dogo, macho sasa yanaelekezwa kwa Kocha Mkuu, Steve Barker, ambaye anakabiliwa na kazi kubwa ya kufanya maamuzi sahihi ya nani aanze katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaochezwa kesho.
Wachezaji waliopata leseni za kucheza ni Clatous Chama, Nickson Kibabage, Libasse Gueye, Djibrilla Kassali na Ismael Toure, ambao wote wamesajiliwa kikamilifu na sasa wako tayari kutumika kulingana na maamuzi ya benchi la ufundi linaloongozwa na Barker.
Akizungumza kuhusiana na suala hilo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wachezaji wote waliosajiliwa katika dirisha dogo tayari wamepata leseni zao na wanaruhusiwa kucheza mchezo wa kesho.
“Kama Kocha Steve ataona kuna haja ya kuwatumia wachezaji wote watano katika mchezo wa kesho dhidi ya Esperance, atafanya hivyo bila tatizo. Sio hao tu, hata kama tutamsajili mchezaji mwingine hivi karibuni naye atakuwa na sifa ya kucheza,” amesema Ahmed.
Ahmed ameeleza kuwa kwa upande wa Chama na Kibabage, wachezaji hao tayari walikuwa wakicheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini sasa wanaruhusiwa pia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na mabadiliko ya kanuni yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
“Kwa mujibu wa kanuni mpya za CAF Champions League, mchezaji anaruhusiwa kucheza CAF Confederation Cup akiwa na timu moja, kisha akasajiliwa na timu nyingine na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu huohuo, tofauti na ilivyokuwa awali,” ameongeza.
Mabadiliko hayo ya kanuni yamekuwa faida kubwa kwa Simba, kwani yameongeza wigo wa chaguo kwa benchi la ufundi na kuongeza ushindani ndani ya kikosi, huku yakiongeza matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo mgumu dhidi ya Esperance, unaotajwa kuwa mtihani mkubwa kwa Wekundu wa Msimbazi.
The post SIMBA YAPATA NGUVU DHIDI YA ESPERANCE appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/zeJ0vWa
via IFTTT
Post a Comment