BARESI ANA KIBARUA KIZITO KWA TRA UNITED

KUNA mechi mbili za Ligi Kuu Bara zinachezwa leo Ijumaa zikihusisha timu zinazopambana kujiweka pazuri kwenye msimamo, huku KMC iliyoifuata TRA United, ikiwa katika mtego chini ya benchi jipya la ufundi.

KMC iliyoachana na Marcio Maximo, imempa nafasi Mohamed Abdallah ‘Bares’ kuwa kocha mkuu, huku ikiunda upya benchi la ufundi ambalo mbali na Bares, kuna Juma Pweka na Imani Mwalupetelo (Makocha Msaidizi), Raphael Mpangala (Kocha wa Makipa), Abdulwahid Abdallah (Kocha wa Utimamu), Ronald Bugingo (Meneja), Tisho Chuma na Ally Malindi (Madaktari), Dalton Mgala (Mtunza Vifaa).

Hata hivyo, inaingia kwenye mechi hii ikiwa haina huduma ya kiungo Ahmed Pipino na beki Abdallah Said ‘Lanso’ waliojiunga na Singida Black Stars.Daruesh Saliboko ndiye mchezaji anayetazamiwa zaidi katika kuiongoza KMC kupambania pointi tatu kwani timu hiyo iliyofunga mabao mawili, yote yamefungwa na mwamba huyo.

Rekodi zinaonyesha, mechi hii iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora kuanzia saa 10:00 jioni, itakuwa ya tano timu hizo kukutana kwenye ligi.

KMC ambayo haina matokeo mazuri msimu huu ikiburuza mkia katika ligi ikikusanya pointi nne baada ya kucheza mechi tisa, inapocheza ugenini dhidi ya TRA United ambayo zamani iliitwa Tabora United, haijawahi kupoteza.

Katika mechi mbili KMC ilizoifuata TRA United, imeshinda 1-0 na nyingine ikitoka 0-0, hivyo rekodi hiyo inaweza kuwabeba leo, lakini inapaswa kujipanga kisawasawa kwani msimu huu haijashinda mechi yoyote ya ugenini, imepoteza zote nne.

TRA inayokamata nafasi ya kumi na pointi tisa kabla ya mechi ya jana, msimu huu haijapoteza katika uwanja wa nyumbani, imecheza mechi tatu, imeshinda moja na sare mbili, hivyo mtanange huu utakuwa wa aina yake.

Mechi tano za mwisho kwenye ligi, imeshuhudiwa TRA ikikusanya pointi saba kati ya 15, ikishinda mbili dhidi ya Singida Black Stars (3-1) na Tanzania Prisons (1-0), imepoteza idadi kama hiyo dhidi ya Mtibwa (2-1) na JKT Tanzania (1-0), huku sare ikiwa moja dhidi ya Mashujaa (0-0).

KMC katika mechi tano za mwisho ligi kuu, imekusanya pointi moja ilipotoka 0-0 dhidi ya Mtibwa, huku ikipoteza nne dhidi ya Pamba Jiji (3-0), JKT Tanzania (1-0), Yanga (4-1) na Fountain Gate (1-0).

Katika mechi zao nne walizokutana kuanzia msimu wa 2023-2024, KMC imeshinda mbili, TRA United ikipata ushindi mara moja, sare pia moja. Matokeo yapo hivi; TRA 0-1 KMC, KMC 0-2 TRA, KMC 4-2 TRA na TRA 0-0 KMC.

Saa 1:00 usiku, Namungo itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi, huku ikisubiriwa kwa hamu kuona Wagosi Wa Kaya wakipata ushindi wa kwanza nyumbani kwa Namungo tangu mara ya mwisho kufanya hivyo Juni 20, 2022 iliposhinda 1-0.

Coastal inayofundishwa na Mohamed Muya, inakwenda kucheza dhidi ya Namungo ikitoka kufungwa 3-0 na Azam.

Rekodi zinaonyesha, Coastal imekutana na Namungo mara 12, imeambulia ushindi mara mbili pekee na zote ikiwa ugenini. Ilifanya hivyo Novemba 22, 2019 iliposhinda 3-1 katika msimu wa kwanza Namungo kucheza Ligi Kuu Bara, kisha ikarudia Juni 20, 2022 katika ushindi wa 1-0.

Namungo imekuwa mbabe mara tano matokeo yakiwa Coastal 0-2 Namungo (Septemba 17, 2024), Namungo 1-0 Coastal )Aprili 17, 2024), Namungo 1-0 Coastal (Septemba 17, 2022), Coastal 1-3 Namungo (Januari 23, 2022) na Namungo 1-0 Coastal (Septemba 6, 2020). Sare baina yao ni tano ikiwamo ya mwisho zilipokutana uwanjani hapo Februari 23, 2025 matokeo yakiwa 0-0 na ndiyo sare pekee iliyopatikana dimbani hapo. Zingine zilikuwa nyumbani kwa Coastal Union.

Namungo mbali na kuwa na rekodi nzuri mbele ya Coastal Union, lakini mechi tano za mwisho imefanya vizuri ikishinda mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City (1-0) na Dodoma Jiji (2-0). Kabla ya hapo, imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Azam, ikitanguliwa kufungwa 1-0 na Mashujaa, pia ikatoka 1-1 na JKT Tanzania.

Coastal Union tano za mwisho imepoteza mbili mfululizo dhidi ya Azam (3-0) na Yanga (1-0). Ilitoka 0-0 na Mashujaa, iliichapa Mbeya City (2-0) na Matokeo ya 1-1 dhidi ya Fountain Gate.

Gepu la pointi linanogesha mechi hii kwani Coastal yenye alama tano ikishinda kwa tofauti ya mabao matatu, itakaa juu ya Namungo iliyokusanya alama nane.

The post BARESI ANA KIBARUA KIZITO KWA TRA UNITED appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/6mbByPK
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post