UJIO wa kiungo mshambuliaji mpya, Alain Anicet Oura, umeendelea kuwapa matumaini makubwa viongozi wa Simba SC, ambao wanaamini usajili unaoendelea kufanywa utaibua mafanikio makubwa ndani ya klabu hiyo msimu huu.
Akizungumza kuhusu usajili huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema Oura ni mchezaji mwenye ubora na uzoefu unaohitajika kusaidia timu kufikia malengo yake ya ndani na kimataifa.
Ahmed amesisitiza kuwa usajili unaofanywa na Simba hauko wa kukurupuka, bali unazingatia maelekezo ya benchi la ufundi pamoja na mahitaji halisi ya kikosi, ili kuhakikisha kila mchezaji anayesajiliwa anaongeza thamani ndani ya timu.
“Mambo makubwa yanakuja hapa. Oura tumemtoa Ulaya, hadi watu wa huko wanalalamika kuwa tumewapokonya mali,” amesema Ahmed kwa kujiamini, akionyesha imani kubwa waliyonayo kwa nyota huyo mpya.
Oura anasifika kwa uzoefu wake mkubwa barani Afrika, ambapo amewahi kuzitumikia klabu za ASEC Mimosas ya Ivory Coast pamoja na Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, akijijengea jina kama kiungo mshambuliaji mwenye mchango mkubwa uwanjani.
Kabla ya kujiunga na Simba, Oura alikuwa akiichezea IF Gnistan ya Finland, hatua inayothibitisha mchanganyiko wa uzoefu wa soka la Ulaya na Afrika ambao anatarajiwa kuutumia kuipa Simba nguvu mpya katika mashindano yanayokuja.
The post MAMBO MAKUBWA YANAKUJA SIMBA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/KkzdE0I
via IFTTT
Post a Comment