SIKU CHACHE BAADA YA KURUDI NYUMBANI….KOCHA SIMBA ATEMA CHECHE KUHUSU CHAMA….

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker ameshindwa kujizuia kwa kuonyesha kuvutiwa na urejeo wa kiungo fundi raia wa Zambia, Clatous Chama, akisema usajili huo ni hatua muhimu katika kuimarisha kikosi hicho kutokana na uzoefu wake.

Mara ya kwanza, Chama alitua Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, akaondoka Agosti 2021 alipouzwa kwenda RS Berkane, hata hivyo hakudumu sana kwa Wamorocco hao, akarejea Simba Januari 2022.

Julai 2024, Chama alipomaliza mkataba wa kuitumikia Simba, akasajiliwa na Yanga alipodumu msimu mmoja wa 2024-2025, kisha Septemba 2025 akatua Singida Black Stars, kabla ya kurejea Simba Januari 2026.

“Kurudi kwa Chama ni jambo zuri. Anafahamu Simba, anajua jinsi ya kushirikiana na wachezaji wenzake na ni mchezaji mwenye akili kubwa ya kimchezo naamini ataongeza kitu kwenye timu,” alisema Barker.

Kocha Barker aliongeza, ujio wa Chama unaongeza machaguo zaidi katika eneo la kiungo mshambuliaji baada ya kuondoka kwa Jean Charles Ahoua na ni fursa ya kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

“Chama ni mchezaji ambaye anaweza kuongoza na kuhimiza wengine. Hii inatupa imani ya kuwa tunayo timu yenye nguvu na yenye mpangilio mzuri,” aliongeza Barker.

Mbali na Chama, Simba pia imeimarisha ukuta wake kwa kusajili kipa mmoja, Djibrilla Kassali na mabeki wawili, Nickson Kibabage, beki wa kati Ismael Olivier Toure ambaye alikuwa mchezaji huru na winga Msenegal, Libasse Gueye.

Kwa upande wake Chama,alisema; “Ninafuraha kubwa kwa sababu Simba ndio nyumbani, najua nini natakiwa kufanya, nitashirikiana na wachezaji wenzangu kuhakikisha tunaisaidia timu kufanya vizuri.”

“Siku zote hakuna jambo bora kama kurejea nyumbani ninachoweza kuahidi kwa mashabiki wa Simba ni kujituma na kufanya kila ninachoweza kwa ajili ya kuisaidia timu.”

Akiongelea urejeo wa Chama Simba, kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohamed Badru alisema; “Sidhani kama kuna kiungo mbunifu kama Chama kwa kuangalia miaka mitano iliyopita niliona hata wakati akiwa Singida bado alikuwa bora, naona ana uwezo bado wa kuisaidia Simba kutokana na hali waliyonayo kwa sasa.”

Kwa muda aliokuwa Simba, Chama alipiga asisti 60 akicheza jumla ya mechi 183 za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

The post SIKU CHACHE BAADA YA KURUDI NYUMBANI….KOCHA SIMBA ATEMA CHECHE KUHUSU CHAMA…. appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/bW8JOqi
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post