KLABU ya Yanga imeweka wazi mkakati kabambe wa kufanya maboresho ndani ya kikosi chao kuelekea dirisha dogo la usajili, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni kuzingatia mapendekezo na ripoti ya benchi la ufundi.
Uongozi umejipanga kuhakikisha wanarekebisha maeneo yaliyoonyesha changamoto katika mzunguko wa kwanza wa ligi na mashindano ya kimataifa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema licha ya ufinyu wa muda na changamoto za kupatikana kwa wachezaji wenye ubora unaotakiwa kipindi hicho, bado klabu imejipanga kufanya kazi kubwa ili kuhakikisha matakwa ya benchi la ufundi yanatekelezwa.
“Wachezaji wazuri huwa wachache dirisha dogo, inahitaji umakini mkubwa katika kufanya maamuzi. benchi la ufundi limekabidhi ripoti kamili yenye mapendekezo mahsusi ya maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu, tayari uongozi unaifanyia kazi kwa karibu ili kuhakikisha kocha anakipata anachohitaji kwa wakati,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuaa lengo ni kuona timu inaendelea kuwa imara na yenye ushindani mkubwa. mipango ya Yanga haiishii tu kwenye usajili wa kikosi cha wakubwa, bali pia inaelekezwa kwenye mradi wao wa Yanga Soccer School ambao umeendelea kukua kwa kasi na kuonyesha matunda yake.
“Hii ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kujenga msingi imara wa vipaji ndani ya klabu,” amesema Ofisa Habari huyo.
Amesema Yanga Soccer School kwa sasa inazidi kupanuka katika maeneo mbalimbali nchini, ikitoa nafasi kwa vijana kupata mafunzo ya msingi ya soka chini ya wakufunzi mahiri. Lengo ni kuona klabu inakuwa na chanzo cha kujitosheleza cha wachezaji chipukizi kwa siku zijazo.
Kamwe ameongeza kuwa uwekezaji huu wa vijana ni mkakati madhubuti wa kuhakikisha Yanga inakuwa na kikosi endelevu, ambacho kitatoa wachezaji bora watakaoingia kwenye kikosi cha kwanza bila gharama kubwa za usajili. Hii ni njia ya kisasa ya kuimarisha klabu kwa muda mrefu.
Yanga imeonyesha dhamira thabiti ya kujiimarisha ndani na nje ya uwanja, kuweka mikakati ya muda mfupi kupitia usajili wa dirisha dogo, na mikakati ya muda mrefu kupitia mradi wa kukuza vipaji.
The post YANGA NA SIRI NZITO YA DIRISHA DOGO WAJIPANGA….. appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/2DTYRSB
via IFTTT
Post a Comment