KLABU ya Simba imejikuta ikipokea maombi mengi ya makocha kutoka maeneo mbalimbali duniani baada ya kutangaza nafasi ya kuinoa timu hiyo kufuatia kuondoka kwa Dimitar Pantev.
Taarifa zinaeleza kuwa jumla ya makocha 240 wamewasilisha maombi yao, jambo linaloonesha ukubwa wa jina na mvuto wa klabu hiyo kwenye ramani ya soka la Afrika.
Katika idadi hiyo kubwa ya maombi, imebainika kuwa ni makocha 136 pekee ndio waliokidhi vigezo vya CAF vinavyotakiwa kwa kocha mkuu wa timu shiriki CAF Champions League.
Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na leseni ya CAF ‘A’ au UEFA Pro, ambavyo ni viwango vya juu kabisa katika ukufunzi wa soka.
Miongoni mwa majina yaliyovutia hisia za wengi ni lile la kocha Romain Folz, kocha aliyewahi kufanya kazi kwenye klabu hasimu ya Yanga SC. Folz, ambaye ana rekodi ya kufundisha kwenye ligi mbalimbali barani Afrika, anatajwa kuwa mmoja wa makocha wa kigeni walioingia kwenye mchujo wa Simba kuelekea kutafuta top 5 kutoka orodha ya makocha 136.
Kuonekana kwa jina la Folz kwenye orodha hiyo kumekonga vichwa vya habari kutokana na historia yake ndani ya Yanga na namna alivyowahi kuwa kipenzi cha baadhi ya mashabiki kwa mtazamo wake wa soka la kushambulia. Kuna wanaoamini uzoefu wake kwenye ligi ya Tanzania unaweza kuwa faida kwa Simba ikiwa atapewa nafasi.
Mbali na Folz, majina mengine makubwa yaliyoainishwa ni pamoja na Erick Tinkler, Honor Janza, Nikodimos “Nikki” Papavasileiou, Hubert Velud na Amine El Lkarma. Kila mmoja kati ya hawa anakuja na rekodi na falsafa tofauti zinazoweza kuongeza ushindani kwenye mchakato wa kumpata mrithi sahihi wa Dimitar Pantev.
Uongozi wa Simba umeeleza kuwa mchujo unaendelea kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha klabu inapata kocha mwenye uwezo wa kurejesha heshima ya timu ndani na nje ya nchi. Hatima ya nani ataukabidhi mikoba ya kukinoa kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi inatarajiwa kujulikana mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa hatua za mwisho.
Mashabiki wa soka nchini kwa sasa wanasubiri kwa hamu kuona iwapo kweli kocha aliyewahi kukalia benchi la Yanga atavuka mchujo na kuibuka chaguo la mwisho la Simba, jambo ambalo bila shaka litazidisha ladha ya ushindani kwenye soka la Tanzania.
The post KOCHA WA YANGA KUIBUKIA MSIMBAZI appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/svznTFI
via IFTTT
Post a Comment