MASHABIKI wa Simba bado hawaamini kilichoikuta timu hiyo katika mechi za kimataifa msimu huu ikiwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba imeshacheza mechi mbili za Kundi D na zote imepoteza mbele ya Petro Atletico de Luanda ya Angola nyumbani na Stade Malien ya Mali ugenini.
Matokeo hayo yameifanya kuwa mkiani katika kundi hilo lenye mabingwa wa zamani, Esperance ya Tunisia pia.
Kinachowachanganya wanasimba ni namna timu imekuwa ikitengeneza nafasi za mabao, lakini walishindwa kubadilisha kuwa mabao.
Tatizo la ukosefu wa umakini na ubunifu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, ndiyo imeonekana kuigharimu na kuleta hofu inaweza kukwama kwenda robo fainali.
Safu hiyo ya ushambuliaji ya Simba inaundwa na nyota kadhaa wakiwamo Jonathan Sowah, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ na Steven Mukwala mbali na viungo washambuliaji mahiri ambao wameshindwa kufanya mambo kila wakiwa ndani ya 18 za lango la wapinzani.
Hilo limejidhihirisha katika mechi mbili zilizopita za Kundi D kwa kufunga bao moja tu, kwa dakika 180 ilizocheza timu hiyo. Mbali na tatizo hilo, pia safu ya ushambuliaji inaonekana bado haina maelewano na mawasiliano mazuri ndani ya uwanja, jambo lililowafanya kushindwa kujipanga na kukaa katika nafasi sahihi wanaposhambulia.
SHIDA YA KUFUNGA
Mengi yanazungumzwa hasa eneo la ushambuliaji kukosa utulivu katika umaliziaji licha ya kutengeneza nafasi nyingi na hili halijaanza chini ya meneja Dimitar Pantev, bali hata kwa kocha aliyepita, Fadlu Davids kabla ya kufanya uamuzi wa kutimka ndani ya kikosi hicho.
Tatizo hili la timu kutengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia, nani alaumiwe?
Novemba 30, 2025 katika mechi dhidi ya Stade Malien, Simba ilipata nafasi nne za wazi ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda kutokana na kushindwa kutumiwa vizuri na kocha ameendelea kulia na safu hiyo ya ushambuliaji kuwa inamuangusha.
Kijumla mechi zote mbili Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 62, ilipiga mashuti 25, kati ya hayo 14 yalipigwa ndani ya boksi na matano yakilenga lango la wapinzani. Pia Simba imekosa nafasi tano kubwa za wazi na jumla ilitengeneza nafasi 21 za wazi za kufunga.
UKUTA MBOVU
Upungufu kadhaa wa ulinzi unaonekana kuwa sababu ya Simba kuruhusu mabao ya mapema kwani bao la kwanza lilimkuta mchezaji wa Malien akiwa peke yake akamalizia, bao la pili mchezaji mmoja aliruka juu peke yake na kuparaza mpira wa kichwa uliokwenda moja kwa moja katika nyavu za kipa Yakoub Suleiman.
Kipindi cha pili, Simba ilibadilika ikaingia na kasi ya kuonyesha kuhitaji mabao ya kusawazisha na haikuwa na bahati zaidi ya kupata bao la moja la kufutia machozi na faida ya mwamuzi wa pambano ambaye alipunguza idadi ya mabao baada ya kutotoa faida kwa Stade Malien ambayo ilifanikiwa kuingiza mpira nyavuni na kulikataa kwa kutaka watumie faida ya pigo la penalti ambalo liliokolewa na kipa Yakoub na kuwa kona isiyozaa bao.
Changamoto ya ukabaji mbovu, huenda ilisababishwa na wachezaji wenyewe baadhi yao walioanza katika mechi hiyo wakiwa hawajiamini, hivyo kusababisha wakose utulivu walipokuwa na mpira na walijikuta katika wakati mgumu zaidi pale mstari wa mbele wa Stade Malien ambao ulikuwa na wachezaji wengi nguvu na utimamu mzuri wa mwili ulipowafuata kwa kasi kubwa ili kujaribu kuwatengenezea presha na wasiwasi.
Udhaifu mwingine wa Simba ulikuwa ni kuachia mianya mingi kwa wapinzani wao lakini baadhi ya wachezaji wa Wekundu hawakuwa na msaada katika kuutafuta mpira pale walipoupoteza au ulipokuwa katika umiliki wa Malien.
MIFUMO TOFAUTI
Pantev alitambulishwa rasmi kuwa meneja wa Simba, Oktoba 3, 2025 akitokea Gaborone United ya Botswana, hadi sasa bado haijafahamika anatumia mfumo gani kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi hicho cha Msimbazi.
Kocha huyo amekuwa akifanya majaribio kwa kutoa nafasi kwa kila mchezaji na kufanya mabadiliko ya mfumo kutokana na aina ya wachezaji anaowatumia kwa mchezo husika.
Kuna muda anatumia mfumo wa bila mshambuliaji, wakati mwingine anatumia mshambuliaji mmoja na wakati mwingine washambuliaji wawili akifanya, hivyo pia kunakuwa na mabadiliko ya wachezaji kutumiwa katika nafasi tofauti kulingana na mfumo anaotaka kuutumia siku hiyo kutokana na aina ya mpinzani.
Hadi sasa haijafahamika kocha huyo ni muumini wa mfumo gani, lakini haijajulikana kikosi chake cha kwanza ni kipi kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara tofauti na watangulizi wake klabuni.
Kuna utofauti mkubwa wa Jean Charles Ahoua aliyekuwa chini ya Fadlu Davids na Pantev ambaye amekuwa akimtumia katika nafasi tofauti na aliyozoeleka namba 10. Msimu uliopita, Ahoua alikuwa akicheza namba 10, eneo ambalo msimu uliopita alihusika na mabao 25 katika Ligi Kuu Bara akifunga 16 akiwa na kinara na asisti tisa. Safari hii, anapangwa pembeni, wakati mwingine eneo hilo alilozoea.
MAJERUHI
Pamoja na mengi kuzungumzwa, lakini matokeo hayo kwa namna moja au nyingine yanaweza yamechangiwa pia na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wenye uzoefu na ni muhimu kwenye kikosi cha Simba.
Simba inamkosa kipa namba moja ambaye msimu uliopita alimaliza na clean sheet 19 na kumweka katika nafasi ya kutwaa tuzo ya kipa bora wa ligi, Moussa Camara aliyefanyiwa upasuaji wa goti.
Lakini ukimuondoa kipa huyo ambaye msimu uliopita timu hiyo ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika aliisaidia kucheza fainali na kwa msimu huu hajacheza mechi hata moja hatua ya makundi kutokana na changamoto ya goti na kutoa nafasi kwa Yakoub ambaye hana uzoefu na michuano hiyo.
Ukiondoa eneo la kipa, Simba pia inakosa huduma ya beki wa kati Abdulrazack Hamza anayesumbuliwa pia na majeraha tangu alipoumia katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao Yanga na Wekundu hao kukubali kichapo cha bao 1-0.
Kukosekana kwa Hamza kumetoa nafasi kwa beki mpya, Wilson Nangu ambaye pia hana uzoefu wa mashindano ya kimataifa kutumika sambamba na Rushine De Reuck au Chamou Karaboue.
Mbali na nyota hao wawili ambao walikuwa panga pangua kikosi cha kwanza akiwemo Yusuf Kagoma ambaye pia haijafahamika ana shida gani kutokana na kukosekana katika mechi mbili zilizopita za makundi, pia Simba ina majeruhi mwingine, Mohamed Bajaber ambaye tangu amesajiliwa hajapata nafasi ya kucheza mechi hata moja.
Kwa maana hiyo, vigogo hao vya soka nchini wanapaswa kuvuta subira na kurekebisha dosari zilizo ndani ya uwezo wao kisha kujipanga vyema kabla ya kukutana na Esperance katika mechi mbili mfululizo mapema mwakani kama inataka kwenda tena robo fainali.
The post UKWELI MCHUNGU…..MATATIZO MAKUBWA YA SIMBA NI HAYA 4….’WAKISOLVU’ HAPA …KICHEKO KINARUDI.. appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/Fd2q75m
via IFTTT
Post a Comment