MTENDAJI Mkuu wa Klabu ya Simba, Zubeda Sakuru, amesema uongozi wa klabu hiyo umejipanga kutumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi kama fursa muhimu ya kuwarejeshea furaha mashabiki wa Simba waliyoikosa kwa muda mrefu kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya mashindano.
Zubeda amesema mashindano hayo yana umuhimu mkubwa kwa klabu hiyo kwani yanakwenda sambamba na malengo ya msimu huu, ambapo Simba imelenga kufanya vizuri katika kila michuano inayoshiriki ili kurejesha hadhi yake ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa benchi la ufundi kwa kushirikiana na uongozi limejiandaa kikamilifu kuhakikisha timu inanufaika na mashindano hayo, si kwa lengo la kutwaa ubingwa pekee, bali pia kuandaa kikosi imara kwa ajili ya changamoto kubwa zinazokuja.
Kwa mujibu wa Zubeda, Kombe la Mapinduzi linatumika kama sehemu ya maandalizi kuelekea michuano ya kimataifa, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kuanza tena Januari 2026, ambapo Simba itahitaji kuwa katika kiwango cha juu.
“Licha ya kwamba tunahitaji kulibeba Kombe la Mapinduzi, lakini michuano hii inatupa nafasi nzuri ya kujiandaa na michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Zubeda, akisisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika maandalizi ya muda mfupi na mrefu.
Ameongeza kuwa kocha mkuu, Steve Barker, atanufaika zaidi na mashindano hayo kwa kupata fursa ya kulitathmini kikosi chake kwa undani, kujua kiwango cha wachezaji na kuona namna wanavyotekeleza maelekezo ya kiufundi uwanjani.
Zubeda amesema michuano hiyo pia itatoa picha halisi ya maeneo yanayohitaji maboresho ndani ya kikosi, jambo litakalomsaidia kocha pamoja na uongozi kupanga mikakati sahihi ya kuimarisha timu.
Kwa ujumla, amesema matarajio ya Simba katika Kombe la Mapinduzi ni makubwa, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuijenga timu imara, yenye ushindani na itakayowapa mashabiki furaha na matokeo chanya katika mashindano yote yanayokuja.
The post JIWE MOJA KUUWA NDEGE WAWILI SIMBA SC appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/Xt0FzC7
via IFTTT
Post a Comment