Yanga yakana kumsamehe Kagoma
Baada ya kusambaa kwa taarifa ambayo ilidaiwa kutolewa na Menejiment ya mchezaji Yusuph Kagoma wakiishukuru klabu ya Yanga kwa kumsamehe mchezaji huyo ambaye alipelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF kutokana na madai ya kimkataba, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe amekanusha taarifa hiyo na kusisitiza kuwa Shauri kati ya klabu na mchezaji huyo bado lipo katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF)
"Hii taarifa ni ya uongo na hatujui aliyetengeneza alikuwa na dhamira gani hakuna taarifa kutoka Yanga kwamba tumemsaheme mchezaji yeyote wala makubaliano yoyote"
"Ni kweli lipo shauri Kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji la klabu ya Yanga likimuhusu mchezaji Yusuph Kagoma na taarifa ni kwamba Kamati imekutana na kufanya maamuzi ya kumsimamisha mchezaji asiendelee kutumia Kwenye mechi za timu yake"
"Kamati yenyewe inashangaa kuona mchezaji bado anatumika huku ana shauri lake chini ya kamati hiyo, nafikiri wadau na wachambuzi wa mpira wa miguu watakuwa na nafasi nzuri ya kutuelezea na kutuchambulia jambo hili," alisema Kamwe
Taarifa hiyo iliyodaiwa kutolewa na Menejiment ya Kagoma ilisambaa jana ikiwa ni takribani wiki moja tangu Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga Dk Mwigulu Nchemba (MB) ambaye pia ni Waziri wa Fedha kuutaka uongozi wa Yanga kumsamehe mchezaji huyo anayedaiwa kusaini mkataba wa kuitumikia Yanga pia akipokea sehemu ya malipo kabla ya kwenda kujiunga na Simba
Taarifa kuhusu sakata la usajili wa mchezaji huyo imebainisha kuwa Yanga ilifuata taratibu zote za kumsajili ikiwa ni pamoja na kununua mkataba wake wa mwaka mmoja uliokuwa umebaki na Singida Fountain Gate wakati Simba walimfuata mchezaji na kumsainisha mkataba pasipo kuwasiliana na Yanga wala Singida FG
No comments:
Post a Comment