Mgambo, ofisa mtendaji wadaiwa kuua mwanafunzi - EDUSPORTSTZ

Latest

Mgambo, ofisa mtendaji wadaiwa kuua mwanafunzi



Moshi/Siha. Ofisa mtendaji katika kata moja wilayani Siha mkoani Kilimanjaro na mgambo, wanadaiwa kuwatembezea kipigo wanafunzi wanne na kusababisha kifo cha mmoja wao anayesoma kidato cha pili.

Marehemu ambaye ametajwa kuwa ni Bright Arnold (14) na wanafunzi wenzake watatu wa shule ya sekondari Fuka wilayani Siha, wanadaiwa kupigwa ndani ya ofisi ya mtendaji huyo wa kata wakituhumiwa kuiba viatu.

Taarifa za mashuhuda zinaeleza wanafunzi hao walifungiwa katika ofisi ya mtendaji huyo hadi wananchi walipoingilia kati lakini wakati huo marehemu alikuwa hawezi kutembea na baadaye kupoteza fahamu.

Aliwahishwa hospitali ya Rufaa ya KCMC, lakini akafariki saa chache baadaye.


 
Ndugu, mashuhuda wafunguka

Akizungumza na Mwananchi, Ruth Munuo ambaye ni mama mkubwa wa marehemu alidai siku ya tukio Juni 17, 2022 akiwa anatoka kwenye shughuli zake, alipata taarifa za mwanawe huyo kuchukuliwa na mgambo na kupelekwa ofisi ya kata.

“Walimchukua wakidai ameiba raba na alikiri kuzichukua na kuonyesha zilipo, lakini walimpiga wakimtaka aonyeshe wenzake, kwa kweli alipigwa kipigo ambacho hakustahili mtoto hata kama alikuwa na makosa,”alidai.

Aliongeza: “Jambo la kusikitisha ni kwamba tukio hili lilifanyika katika ofisi ya kata ambako tunajua ndiko kimbilio letu wanyonge, na nilipofika nilimkuta amevimba kila mahali na ana hali mbaya sana.’’


Kwa upande wake, Elisifa Mrang’u ambaye ni shangazi wa marehemu, alidai siku hiyo saa 5 asubuhi, alielezwa kuwa kuna kijana aliyekuwa ameongozana na mgambo wa kata, walimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka ofisi za kata akidaiwa kuiba viatu.

“Nikiwa sielewi chochote kwenye saa 11:00 jioni nilipita ofisi hizo, nikawaona watu na wanafunzi wakichungulia dirishani na mlangoni, nikauliza kuna nini nikaambiwa kuna wanafunzi wameiba wanapigwa.”

“Nikaambiwa alipoulizwa alikiri na alimtaja mtu aliyekuwa navyo, lakini kaniambia mgambo hao waliendelea kumpiga na kumtaka ataje vitu vingine walivyoiba na watoto wengine wanaoshirikiana huku wakiendelea kumpiga.”

Alidai kuwa aliamua kusogea kuangalia akamuona mtoto wao (marehemu) akipigwa na mgambo wawili na mtendaji kata wakitumia marungu na mateke.


 
‘‘Ni tukio nililolishuhudia mwenyewe.Nilishuhudia akipigwa na walikuwa watoto wanne...,’’ alisema.

Baada ya kichapo

Alidai walipotoka nje watoto watatu waliweza kusimama, lakini Bright hakuweza kusimama kabisa kwa kuwa alikuwa ameumizwa sana kwenye magoti na kichwani.

Alibebwa na wananchi na kukimbizwa hospitali Kibong’oto kwa pikipiki,”alidai ndugu huyo.

Inadaiwa baadaye hali yake ilizidi kuwa mbaya akahamishiwa Hospitali ya KCMC na kesho yake alifariki dunia na kusema, tukio hilo limemuumiza sana maana wangeweza kumpeleka kwenye vyombo vya sheria kama amefanya kosa.


Naye mjomba wa Marehemu, aitwaye Baltazary Mmary alilaani kitendo hicho na kueleza kuwa ni tukio la kikatili na kinyama na linapaswa kukemewa na vyombo vyenye mamlaka ili kuepusha tena tukio kama hilo kutokea.

Kauli ya viongozi Siha

Juni 17, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alikaririwa akisema ofisa mtendaji pamoja na mgambo, walikuwa wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwapiga watu kadhaa na kusababisha Bright kulazwa KCMC.

Lakini jana na juzi alipotafutwa ili kuzungumzia kifo cha Bright aliyekuwa amelazwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) kuwa amefariki, simu yake iliita bila majibu na wakati mwingine kupokelewa na mlinzi wake.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Thomas Apson alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kusema bado hajapata taarifa kamili kuhusiana na kilichotokea na kuomba kupewa muda ili kulifuatilia kwa karibu na kubaini chanzo cha kifo hicho.

“Kifo hiki kinauma nami nimeumia sana, lakini kifo hiki kina mambo mengi, na sijapata taarifa sahihi wala taarifa ya daktari inayoeleza chanzo chake. Naomba muda nilifuatilie niweze kupata taarifa sahihi,”alisema mkuu huyo wa wilaya.


Mwananchi




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz