REAL Madrid ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) na Supercup ya Hispania msimu huu wa 2021/22, na mafanikio yao yana siri nyuma yake.
Baada ya msimu wa 2020/21 ambao ulimalizika bila mataji na baada ya kuondoka kwa watu wawili muhimu kikosini – Zinedine Zidane na Sergio Ramos – Real Madrid ilionekana itakuwa na msimu mbovu unaofuata, hasa baada ya kushindwa kumsajili Kylian Mbappe katika usajili wa majira ya joto yaliyopita.
Lakini miezi tisa baadaye, stori ni nyingine. Real Madrid imeufunga msimu kwa mataji matatu kati ya manne iliyokuwa inawania.
Toni Kroos na David Alaba wametoa mitazamo yao kuhusu mafanikio yao hayo.
“Kushinda Ligi ya Mabingwa daima ni ngumu na mara zote haitabiriki,” anasema Kroos alipozungumza na Sport 1.
“Pengine mwaka huu ilikuwa ngumu zaidi lakini kwangu mimi makombe yote matano (ya Ligi ya Mabingwa Ulaya) niliyoshinda yana thamani sawa. Lakini kama nikiwa muwazi, pengine ni Ligi ya Mabingwa ndilo kombe ambalo nilikuwa sitarajii kulitwaa kati ya matano.”
Ubora wa Casemiro, Modric, na Kroos
Kroos, sambamba na Luka Modric na Casemiro, waliongeza tu sifa zao kama moja ya kombinesheni bora zaidi za kiungo kihistoria. Ubora wao hauonekani kuwa unaelekea mwisho.
“Samahani, (ubora huu) hautafikia mwisho,” anasema Kroos huku akicheka. “Hapana, kiukweli, bila shaka tunataka kuendelea kucheza katika levo hii.
“Kila mmoja wetu anajua nini wengine wanaweza kufanya na nini hawawezi kufanya. Hiyo inatusaidia sana, hasa kwenye mechi kubwa ambazo tumekuwa tukicheza.
“Tulikuwa na vijana wawili kwenye timu msimu huu, (Fede) Valverde na (Eduardo) Camavinga, ambao kiuhakika walitusukuma, iwe ni kwenye benchi au kwenye kuanza mechi.
“Hii ni muhimu na itakuwa muhimu zaidi na zaidi. Kwa sababu kwa wakati fulani, watatakiwa kuchukua nafasi zetu moja kwa moja.”
Alaba, ambaye amemaliza msimu wake wa kwanza Santiago Bernabeu kwa mafanikio, naye alitoa ya moyoni kuhusiana na mafanikio ya Real Madrid msimu huu.
“Kuna sababu nyingi zilizochangia,” anasema Alaba. “Ubora, morali…. sisi ni timu yenye wachezaji wazuri, lakini pia timu ambayo daima inaamini kwenye kutafuta ushindi hadi (dakika ya) mwisho.
“Tunafanya kila linalowezekana kushinda. Real Madrid imeonyesha njaa yake ya mafanikio kwa muda uliopita na muda huu. Na sasa nami nikiwemo kwenye kundi, nina furaha sana kuwa sehemu ya timu hii.”
Courtois na Ancelotti
Alaba, raia wa Austria, akiendelea kufunguka, hakusahau mchango wa Thibaut Courtois langoni msimu huu.
“Ambacho Thibaut amefanikisha hakika kinashangaza, na amekifanya kwa kipindi chote cha msimu,” anasema Alaba. “Ametuokoa mara nyingi sana.”
Kitu ambacho Kroos na Alaba wanakubaliana wote ni madhara ya kocha Carlo Ancelotti katika timu hiyo.
“Carlo ni kocha maalum sana,” anasema Kroos. “Ni mtulivu sana na anaileta hiyo kwenye timu.”
“Huwezi kuona utulivu wake mara kwa mara katika kazi yake na sisi tunafanya hivyohivyo,” anaongeza Alaba.
The post Kroos, Alaba Wafichua Siri ya mafanikio ya Real Madrid appeared first on Global Publishers.
No comments:
Post a Comment