Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania imetangaza kusitisha msako wa Ndege iliyopotea ikiwa na Rubani Samweli Balina Gibuyi baada ya kutopata chochote kwenye msako huo uliofanyika kwa wiki kadhaa kwa kutumia anga na ardhini kuyatazama maeneo yote ambayo yalikua yanatajwa kuwa huenda angekutwa huko.
Ndege hiyo ndogo iliyosajiliwa nchini Tanzania kama 5H-MXO aina ya BatHawk inayomilikiwa na PAMS Foundation iliripotiwa kupotea tarehe 18 October 2021 baada ya kuondoka katika kiwanja kidogo cha Matemanga kilichopo Wilayani Tunduru saa tisa alasiri kuelekea kiwanja kidogo cha Kingupira kilichopo Hifadhi ya Selous kwa lengo la kufuatilia mienendo na usalama wa wanyamapori hasa Faru weusi.
Ndege hiyo ilipoondoka ilikuwa na Rubani pekee na haikuwasiliana na kituo chochote cha kuongozea ndege wala haikuweza kuonekana kwenye mitambo ya kuangazia ndege kwa sababu ilikuwa ikiruka chini sana na sasa Taarifa ya Mamlaka ya anga Tanzania imesema utafutaji wake sasa unasitishwa mpaka pale itakapopata taarifa zinazoashiria upatikanaji wa ndege au Rubani wake.
Post a Comment