Daraja la Tanzanite Kuanza Kutumika Desemba - EDUSPORTSTZ

Latest

Daraja la Tanzanite Kuanza Kutumika Desemba



MRADI wa ujenzi wa daraja jipya la Tanzanite unaosimamiwa na serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), umefikia asilimia 93, huku Desemba mwaka huu likitarajiwa kuanza kutumika.

Akizungumza wakati akikagua na kushiriki uwekaji wa zege kuunganisha kipande cha mwisho cha daraja, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila, alisema daraja hilo lipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Alisema Desemba mwaka huu, daraja litaanza kutumiwa na magari pamoja na waenda kwa miguu.

Akifafanua baadhi ya faida za mradi, Mativila alisema changamoto ya msongamano wa magari inayolikabili daraja la awali katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, itakuwa historia.


"Ule msongamano mkubwa uliokuwa ukilikabili daraja dogo la zamani la Salander hautakuwepo tena, kwa sababu daraja hili jipya litatumika pamoja na la zamani," alisema.

Alisema mbali na kupunguza msongamano, uzuri wa daraja jipya la Tanzanite utakuwa kivutio cha utalii, hata mgeni akitoka mbali atatamani kwenda kuliona daraja hilo.

Mativila alisema kwa sasa wanafanya mawasiliano na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani Kinondoni ili kuboresha barabara zao kutokea Coco Beach kwenda hoteli ya SeaCliff hadi Slip Way.

"Katika barabara tunazounganisha kuna hii ambayo tumejenga ambayo inaishia Coco Beach, lakini tunawasiliana na wenzetu wa Tarura Kinondoni, ili waboreshe barabara zao kutoka Coco kwenda Sea Cliff izunguke kuja Slip Way ili watu wanaokwepa msongamano wawe na namna ya kupita hadi kutokea nje ya mkoa au kuingia," alisema.

Mradi wa daraja jipya la Tanzanite unatekelezwa na Kampuni ya Uhandisi ya GS Engineering kutoka Korea Kusini, Mhandisi Mshauri ni Kampuni ya Yooshin Engineering kutoka Korea Kusini ikishirikiana na Afrisa Consulting ya Tanzania.

Aidha, mradi unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 243 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea na fedha za Serikali ya Tanzania.




Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz