Utata Mauaji Askari Wanne - EDUSPORTSTZ

Latest

Utata Mauaji Askari Wanne

Katika tukio hilo ambalo watu wengine sita wamejeruhiwa, kijana mwenye silaha ambaye baada ya kufanya mauaji hayo aliuawa na Jeshi la Polisi, anadaiwa kufika eneo hilo na kuanza kufyatua risasi ovyo na kusababisha taharuki kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Kutokana na tukio hilo, Rais Samia ametoa pole kwa Jeshi la Polisi na familia za askari polisi watatu na askari mmoja wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA waliopoteza maisha baada ya mtu huyo mwenye silaha kuwashambulia.Kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter jana, Rais ameliagiza Jeshi la Polisi kuchunguza kwa kina tukio hilo huku akieleza kuwa mtu huyo amedhibitiwa na hali ni shwari. Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alisema mtu huyo aliwaua askari wawili.

"Aliwapiga risasi wote wawili, akaingia barabara kuu akawa anatamba na SMG naye akapigwa risasi na askari wetu, askari wetu wamefariki na yeye huyu bwana amefariki.

"Tunaendelea kufuatilia kujua namna gani, lakini challenge (changamoto) tuliyonayo ni kwamba kama mnavyojua kule Msumbiji kuna shida.

“Majeshi yetu yapo kule, ni suala la kujipanga, tumepoteza askari wetu wawili lakini huyu Bwana aliyefanya mauaji hayo tunataka kujua ametoka wapi, ni nani? Baadaye nitawapa taarifa," aliahidi. Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi, Liberatus Sabas, alisema wakati askari wakiwa kazini, alifika mtu huyo akawashambulia kwa silaha aina ya bastola kisha akachukua silaha mbili akaanza kurusha risasi ovyo kuelekea Ubalozi wa Ufaransa.

Alisema alipofika ubalozini kuna kibanda akajibanza na kuanza kufyatua risasi ovyo na kuua askari wanne na kujeruhi watu sita ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). 

"Uchunguzi utabaini (sababu), tumeshaanzisha timu ya upelelezi na muda sio mrefu tutakamilisha,

" alisema. WALIOSHUHUDIAAskari anayefanya kazi Ubalozi wa Ufaransa, ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisimulia kuwa wakati tukio linatokea ilikuwa majira ya saa 5:30 asubuhi ambapo walianza kusikia milio ya risasi ikitokea nje ya geti lao. 

“Sisi tulikuwa ndani, milio ya risasi ilianza kusikika maeneo ya Selander, wakati huo tulikuwa askari wawili wa kampuni na nje walikuwa askari polisi ambao wakati huo walikwenda kudumisha nguvu maeneo ya Daraja la Selander ambao pia wanakujaga hapa maeneo ya ubalozi. 

“Wakawa wameondoka, wamekwenda kule baadaye ndiyo tukasikia hizo sauti za milio ya bunduki wakati hao askari hawapo, tulipochungulia tukaona kuna mashambulio yanaendelea, tukatoa taarifa kwa bosi wetu," alidai. 

Alisema baadaye aliona mtu huyo akikimbilia maeneo ya kibanda cha askari polisi nje ya jengo hilo ndipo baadhi ya askari polisi wakamshambulia wakiwa wanatupiana risasi.


 "Mpaka anauawa yalikuwa ni mashambulizi kati ya askari polisi na huyo mtu ambaye mpaka sasa hatujui alikuwa na shida gani," alisema. 


Shuhuda mwingine, Maziku Mohamed alidai kijana aliyefanya mauaji hayo alitokea eneo la Daraja la Selander, akaingia kwenye kibanda cha askari, akachukua silaha ya askari polisi na kuwajeruhi kisha kwenda eneo la Ubalozi wa Ufaransa. Alidai mtu huyo alianza kurusha risasi akijibizana na askari polisi na kusababisha taharuki eneo hilo, magari yakishindwa kupita.

 "Alikuwa peke yake, ana asili kama ya Kisomali hivi lakini polisi walimzunguka, kwa hiyo kama unavyoona yupo chini," alisema.

 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kilitoa salamu za rambirambi kwa IGP Sirro na familia zilizopoteza ndugu zao kutokana na tukio hilo. “Tunaomba Watanzania wawaombee majeruhi wote ili waweze kupona na kuendelea na majukumu ya kujenga taifa," ilisomeka sehemu ya taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz