Yanga yafunguka Kazi za Manara Baada ya Kumchukua - EDUSPORTSTZ

Latest

Yanga yafunguka Kazi za Manara Baada ya KumchukuaSIKU moja baada ya aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, kutangaza kujiunga na klabu hiyo, mabosi wa Yanga wameweka wazi majukumu ambayo yatafanywa na kiongozi huyo, imefahamika.

Manara alitambulishwa rasmi kuhamia Yanga juzi, lakini haikuelezwa atakuwa katika nafasi gani ndani ya klabu hiyo ambayo msimu ujao itashiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa, alisema wanachama na mashabiki wamekuwa na wasiwasi juu ya kazi atakazofanya Manara kutokana na uwepo wa Ofisa Mhamasishaji, Antonio Nugaz na Ofisa Habari, Hassan Bumbuli.

Mfikirwa alisema Manara atashughulika zaidi katika idara ya kuhamasisha mashabiki na hiyo itasaidia kuiimarisha klabu yao kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.

"Wakati tunamtangaza Haji (Manara) pale Serena jana (juzi) hatukusema anakuja kufanya kazi gani hasa, lakini niseme uongozi upo makini na haujakurupuka kumchukua Haji, kuna majukumu yapo na ataenda kuyafanyia kazi hasa kutokana na mabadiliko ya klabu yanayofanywa sasa, kutoka katika mfumo wa sasa na kwenda mfumo mpya na wa kisasa zaidi, hatoingiliana na Nugaz na Bumbuli" alisema Mfikirwa na kuendelea.


"Katika mabadiliko ambayo tunayafanya kwa sasa kuna suala la ‘fan base', hapa tunahitaji mtu wa kushawishi mashabiki waingie kwenye mfumo rasmi wa klabu baada ya kukamilika taratibu zote, kuna mashabiki mikoa mbalimbali ambao klabu inawahitaji, lakini lazima washawishike, hapa ndipo panapohitajika watu au mtu mwenye kujua kushawishi, kuna nani zaidi ya Manara?, ili ni eneo ambalo tunaamini atafanya kazi kubwa sana kwa manufaa ya klabu," alisema Mfikirwa.
Alisema kila mmoja (Nugaz, Bumbuli na Manara), atafanya kazi yake kwa maendeleo ya klabu na hakutakuwa na mwingiliano.

"Mashabiki wauamini uongozi wao, sisi tupo pale (madarakani) kwa niaba yao, hivyo chochote tutakachokifanya ni kwa faida ya timu hivyo hakuna haja ya kuwa na shaka na ujio wa Manara ndani ya Yanga," Mfikirwa alisema.

Naye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Wadhamini wa klabu hiyo kutoka GSM, Hersi Said, alisema Manara amekuja kuongeza 'kitu' ndani ya klabu hiyo.


Hersi alisema wanaamini Manara atailetea mafanikio chanya Yanga na uamuzi wa kumchukua umefanywa na umezingatia maslahi ya klabu yao.

Mapema wakati wa uzinduzi wa jezi mpya, Manara alianza kwa kuwapiga kijembe Simba huku akiwaomba mashabiki, wanachama pamoja na viongozi wa klabu hiyo kumpa ushirikiano ili afanye kazi yake kwa ufasaha na weledi.

"Niliyoyafanya kule (Simba), nilipotoka huku nitayafanya mara elfu moja..., nimekuja kwenye klabu kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, tazama na leo (jana), tunazindua jezi bora zaidi ambayo haina makorokocho, haina pikipiki, haina nazi wala uchafu wowote, hizi ni jezi bora kwa ajili ya timu bora," alisema Manara huku akishangiliwa na baadhi ya mashabiki na viongozi wa klabu hiyo walioudhuria hafla hiyo.

Manara alisema kwa sasa amekuwa na furaha baada ya kupitia 'mambo magumu' na ameishukuru Yanga kwa kumwamini na kumchukua.


Viongozi mbalimbali walihudhuria uzinduzi wa jezi hizo zitakazotumika katika msimu wa 2021/2022 akiwamo Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Wilaya ya Temeke na shabiki wa Yanga, Jokate Mwegelo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani.

Jezi hizo zilizozinduliwa zitatumika katika mechi za nyumbani na ugenini katika Ligi Kuu Tanzania Bara, michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na jezi kwa ajili safari kwa wachezaji, benchi la ufundi na viongozi.
Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz