Manara Ameupiga Mwingi, Ishu Ya Kufatiliwa - EDUSPORTSTZ

Latest

Manara Ameupiga Mwingi, Ishu Ya Kufatiliwa

ALICHOKIFANYA aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, jana Jumatano mbele ya waandishi wa habari pale Hoteli ya Serena, Dar, watoto wa mjini wanakwambia ameupiga mwingi.

 

Jana Manara alizungumza mambo mengi mbele ya vyombo vya habari akiwa na lengo la kuwashukuru viongozi wa Simba, mashabiki wa timu hiyo na kila mmoja aliyekuwa naye karibu kwa muda wote wa miaka sita aliokaa ndani ya klabu hiyo kwa nafasi yake ya ofisa habari.

 

Katika mazungumzo yake hayo, pia Manara alitoa tuhuma nzito kwa baadhi ya viongozi wa Simba, akiwemo Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, huku mara kadhaa akimtaja mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’.Julai 18, mwaka huu, Simba ilitangaza kuridhia Manara kuondoka kwenye nafasi yake hiyo baada ya kuomba kufanya hivyo na nafasi yake kupewa Ezekiel Kamwaga.


KUANZA KAZI

Katika mkutano wake na wanahabari jana, Manara alianza kwa kueleza kwamba: “Nimekuja kuongea kipekee, 2015 mwanzoni bwana Evans Aveva (aliyekuwa Rais wa Simba), ambaye yeye na kamati yake ya utendaji iliniomba niwe msemaji wa Simba ambayo ni taasisi yenye raha.

 

“Nilifanya kazi 2016 na Patrick Kahemele, nilifanya kazi na Crescentius Magori akiwa ni mtendaji wa kwanza, zama zake nilianza kupanda ndege. Kisha Senzo Mbatha, huyu kutoka Afrika Kusini nilijifunza mengi kwao.

 

“Niwashukuru ninyi wanahabari mmenifanya niwe hapa. Nyie mmenitangaza na kunifanya nikajulikana. Serikali pia, mawaziri nao walikuwa wakinipa sapoti.“Aliye mkamilifu juu ya dunia hii ni Mwenyezi Mungu peke yake.

 

Pale ambapo niliteleza kama binadamu ‘I’m sorry’ (samahani). Sijakamilika na sijawahi kukamilika. Ndani ya miaka sita huenda nimefanya ‘press’ (mkutano na waandishi wa habari) nyingi kuliko wengine.

 

MECHI ZA KIMATAIFA

“Nakumbuka mechi moja tunacheza na Al Ahly tumepigwa tano, sasa tukarudi Dar, wakasema tunafanyaje, nikasema acheni kwanza, nikaja na sera mbalimbali.“Nikaja na Do or Die. Nimeleta hamasa. Nadhani kwamba siku moja dunia itanikumbuka. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

 

Akili kubwa ilitumika.“Licha ya kampeni zote lakini sikuwa ninapewa kipaumbele. Ilipokuja neema nimekuwa najigharamia mpaka safari za nje ya nchi. “Mechi dhidi ya Mbabane nakumbuka niliambiwa jina langu halipo. Ikabidi nijigharamie. Nililala kwenye makochi Afrika Kusini. Siku ya mechi kutokana na fitina nikaambiwa nikae chumbani. Matokeo nikawa napata nipo chumbani.

 

ISHU YA MKATABA WAKE

Katika sakata hili la mkataba, Manara anadai kwamba, kwa muda wa miaka sita, mshahara wake ulikuwa ni shilingi laki saba na alikuwa anafanya kazi bila mkataba.Manara anadai kwamba, alipoongea na Mohamed Dewji, akamwambia wataangalia namna ya kufanya ili awe analipwa.“Mimi wakati naingia Simba SC hali yetu kama klabu ilikuwa mbaya, nikaambiwa Haji jitolee kipindi hiki, tutaanza kukulipa baadaye tukipata uwezo, nikakubali huku nikijua aliyekuwepo kabla yangu alikuwa akilipwa.“Mechi za mikoani nilikuwa nakwenda na basi, sikuwa nafanya kazi ya ofisa habari tu, nikifika nitafute hoteli, maji ya kunywa, nimepambana sana.

 

Akili yangu imefanikisha mambo mengi ya kimaendeleo Simba.“Mwaka 2017 mambo yakaanza kuwa mazuri baada ya SportPesa kuingia kutudhamini,” anasema Manara.

 

Manara aliendelea kueleza kwamba, wakati Magori anajiuzulu na kuja Senzo Mbatha, kiongozi huyo raia wa Afrika Kusini akamuita ofisini kwamba Mohamed Dewji na kuambiwa kwamba anatakiwa kuondolewa. “Akaniambia moja ya kazi ambayo aliambiwa aifanye ni kunifukuza kazi. Ila yeye aliniambia hawezi kunifukuza akiomba nifanye naye kazi, tukawa pamoja.”

 

SABABU YA KUENGULIWA SIMBA

Manara anadai kwamba, ishu kubwa iliyomfanya mpaka akaondolewa Simba ni masuala yake ya kimikataba na makampuni mengine nje ya eneo lake la kazi.Maelezo ya Manara ni kwamba, alipewa ofa ya kutangaza bidhaa za Azam, akaenda kumwambia Mo kuhusu ishu hiyo, akamwambia haiwezekani. Hapo akaitwa Barbara na kutakiwa kumpa mkataba wa kutangaza bidhaa za Mo.“Ilipita miezi sita hakuna dili. Nikimpigia Barbara anasema nitakupigia baadaye.”

 

AOMBWA WAVUNJE MKATABA WA AZAM

Manara aliendelea kufunguka kwamba, Mo alimuomba mkataba wake na Azam ambao ulikuwa na kipengele cha kuuvunja lazima shilingi milioni 350 ziwekwe.“Hapo ikawa ngumu, akaniambia anataka abaki na ule mkataba, nikamkatalia. Ndipo ishu ya bwana Hans Pope ilipoibuka.

 

ISHU YA MKATABA WA MILIONI 4

Hivi karibuni, yaliibuka maneno kwamba Manara amekataa kusaini mkataba wenye thamani ya shilingi milioni nne aliopewa na Simba.Kuhusu hilo, mwenyewe amekanusha kwa kusema: “Barbara akaambiwa kwamba anitengenezee mkataba, mshahara wake ulikuwa ni milioni tatu na siyo nne, lakini ukiwa na kipengele kwamba Ayoyote zaidi ya Mohammed Enterprises. Nikashangaa.“Nikasema inakuwaje nisaini mkataba wa milioni tatu halafu lazima nifanye kazi na Mohamed Dewji, nikauliza mimi nimeajiriwa na Simba au Mohamed Dewji. Barbara akaambiwa akarekebishe.“Mwezi wa pili wakarekebisha Barbara akaniita ofisini, safari hii mkataba ulikuwa na ileile milioni tatu, lakini ukiwa na kipengele kwamba siruhusiwi kutangaza bidhaa ambayo ni mshindani na inayoidhamini Simba. Mdhamini mkuu wa Simba ni SportPesa ndiyo maana sitangazi na kampuni nyingine ya betting kwa kuheshimu hilo.”Manara anadai kwamba, baada ya hilo kushindikana, Mo akaanza kubadilika, ndiyo ile roho ya lazima yeye aondolewe ikatokea.

 

HUJUMA SIMBA V YANGA

“Kuelekea kwenye mechi yetu dhidi ya Yanga, Kigoma, nilikuwa natoa sadaka ya Sikukuu ya Idd, saa tatu nilipigiwa simu na Barbara akaniuliza upo wapi? Naambiwa upo Posta, nikamwambia mimi nipo Kariakoo, akasema hapana, wewe upo Posta na Gharib (GSM) unatuhujumu, nikamuacha.

 

“Siku ya pili nikatumiwa meseji kwamba Haji unatuhujumu aliyetuma alikuwa ni Barbara, jana ulikuwa na GSM kisha ukaenda Posta kisha Kigamboni kambi ya Yanga. Sasa nikawa najiuliza nahujumu vipi?

 

“Kweli nilipata hasira, inawezekana nilituma ile voice note. Ningehujumu wakati wa Manji, yaani nahujumu vipi, kwa nini? Mimi sijatuma na sikuwa na namna nilipambana kwa miaka 6 na sina contract (mkataba). Serikali ipo inanisikia sina mkataba wananihujumu. Nimefanya kazi muda wote.

 

ISHU YA KUFUATILIWA

Manara anadai kwamba, aliitwa na Mo akiwa na mtu ambaye alitambulika kama wa usalama, kisha ikaletwa simu akaambiwa kuna muda ilikuwa inasoma yupo Posta, kisha Kigamboni akituhumiwa kwenda kuihujumu Simba kwa viongozi wa Yanga ambao kambi yao ipo Kimbiji, Kigamboni.“Nikamuuliza Mohamed wewe ni nani? Usalama wa taifa, Polisi? Cyber Crime? Wewe kwa sababu una pesa? Kweli nilikuwa ninaenda Kigamboni, lakini nilimuuliza haki hii ya kunifuatilia unaipata wapi? Nimeona wengi wanawafuatilia, naomba Serikali inilinde katika hili.

 

TIMUATIMUA SIMBA

“Nadhani kwenye utawala wa Barbara wafanyakazi 9 ama 10, wametolewa.”Manara aliwataja baadhi ya waliokumbana na joto ya jiwe chini ya Barbara tangu awe mtendaji mkuu wa Simba akiwemo Hashim Mbaga, Arnorld Kasembe,huku Patrick Rweyemamu akiondolewa na kurudishwa.“Barbara hajatimiza miaka 10, ila amefukuza watu wengi. Najua na mimi wanatafuta ili tu wanipe kitu cha kuniweka ndani.

 

MKATABA WA AZAM NA SIMBA

“Januari mwaka huu, Simba kupitia Barbara walisaini mkataba na Azam utakaoisha msimu wa 2022/23 wenye thamani ya shilingi milioni 385 kwa mwaka. “Tumefika mwezi wa sita, Azam walipotaka kuingia mkataba na TFF ambao unazihusu timu zote.

 

Baada ya mkataba ule, watu wa Simba wakasema hawawezi kupewa sawa na Yanga.“Barbara akawapigia watu wa Yanga akawaambia waende kujadiliana na Azam hawawezi kupewa sawa.

 

Wakakaa vikao vitatu sambamba na watu wa Yanga na Azam, mwisho wakakubaliana, Kipindi cha Simba TV na Yanga TV Azam wataweka bilioni 2.4 kwa mwaka ikiwa na nyongeza. Unajua kilichotokea baada ya hapo, bwana mkubwa akakataa.“Yanga wao walikuja kuingia mkataba wa bilioni 34 kwa miaka kumi.”

 

“Mo anasema Azam wanatoa hela ndogo, nikamuuliza wewe unatoa bei gani, ukiangalia jezi zetu zina matangazo mengi, jezi imechafuka za klabu za Sudan, leo hii anasemaje hafanyi biashara!”Manara anadai kwamba, chuki ya bosi huyo mkubwa wa Simba kwa Azam imetengeneza mtego kwake.“Kwa sababu ya kudai haki yangu, nimeonewa, nimedhulumiwa, nawaaga tena mashabiki,” alimaliza Manara ambaye alisema kuwa atarudi kwenye mpira.

WAANDISHI: LUNYAMADZO MLYUKA, ONESMO MILANZI NA JOHARI IDDYDownload our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz