Tanzania Kuanza na Chanjo Nne za Corona - EDUSPORTSTZ

Latest

Tanzania Kuanza na Chanjo Nne za Corona
Wakati sehehena ya chanjo za aina nne ikiwa njiani, Serikali imebainisha makundi yatakayoanza kukingwa maambukizi ya virusi vya corona.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipohojiwa na kituo cha runinga cha Azam juzi, alisema kundi la kwanza kupata chanjo hiyo ni watoa huduma za afya.

Chanjo hizo, alisema zitaanza kuwasili nchini miezi mitatu kutoka sasa “lakini zitakazotumiwa na makundi mengine zitawasili Desemba.”

Profesa Makubi alisema chanjo nne zilizochaguliwa ni kutokana na ushauri wa kamati ya wataalamu iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuuchambua kwa kina ugonjwa wa corona na kuishauri Serikali la kufanya.

“Wataalamu walishauri tutumie zaidi ya chanjo aina moja ili kuwapa nafasi wananchi kuchagua wanayoipenda. Watu watakuwa na uchaguzi wa kuamua mimi nachukua hii au hii, kwa hiyo tunategemea kama mambo yataenda vizuri ndani ya miezi mitatu ijayo tutakuwa tumeshapata chanjo za awali,” alisema.

Profesa Makubi alisema kutokana na mlipuko wa tatu wa virusi hivyo, Serikali itahakikisha makundi yaliyo hatarini, wakiwamo watumishi wa afya wanachanjwa mapema. Alisema wapo watu ambao ni lazima kupata chanjo hiyo, wakiwamo wasafiri na wanaohudhuria mikutano.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya mwaka mmoja wa kifo cha Hayati Benjamin Mkapa, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na corona na inakamilisha taratibu za kuagiza chanjo yake.

“Mwelekeo ni kila atakayehitaji chanjo iwe inapatikana, kama nilivyosema kabla kuwa chanjo hiyo ni ya hiari,” alisema Rais Samia.

Wakati Serikali ikieleza mikakati hiyo, Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania (TMDA), imesema inashiriki kufanya tathmini ya chanjo hiyo kupitia nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo alisema wameimarisha mifumo ya udhibiti kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu ubora, usalama na ufanisi wake.

“Tunayo timu ya wataalamu na mifumo yetu ipo vizuri, tutaichunguza na kujiridhisha ndipo iingie. Tutaendelea kufuatilia kwa ukaribu madhara yanayoweza kusababishwa na chanjo hiyo,” alisema.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja, Dk Abdulrahman Khalfan Said amesema kuna wagonjwa watatu wa corona wamelazwa katika hospitali hiyo iliyopo mjini Unguja.

“Hiyo sio siri, tumeanza kuwapokea wagonjwa wa corona, wapo watatu. Wananchi tuwe na tahadhari kujikinga na kuwakinga wengine,” alisema Dk Said.

Msemaji wa hospitali hiyo, Hassan Makame Mcha alisema wamebadili utaratibu na kupunguza idadi ya ndugu wanaokwenda kuwaona wagonjwa, sita tu kwa sasa kwa siku.


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz