Jeshi la Polisi na Magereza leo wameimarisha ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na wenzake walipofikishwa mahakamani hapo kusomewa mashitaka sita yanayomkabili.
Sabaya tayari amefikishwa mahakamani saa 3 : 07 akiwa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa chumba cha mahabusu ya Mahakama.
Sabaya na wenzake walikuwa wenyewe ndani ya gari la mahabusu huku kukiwa hakuna watuhumiwa wengine.
Kabla ya kushushwa gari hilo kulitanguliwa na magari mawili ya askari polisi waliokuwa na silaha ambapo watu waliokuwa nje ya eneo la mahakama hiyo waliamriwa kutoka nje ya geti wakati watuhumiwa hao wanashushwa katika gari hilo.
Katika shauri hilo la jinai namba 66 la mwaka huu, watuhumiwa wengine ni waliokuwa walinzi wa Ole Sabaya, Daniel Mbura na Sylvester Nyingu maarufu kama Kicheche, Nathan Msuya na Jackson Macha.
Katika kesi hiyo ya unyang'anyi wa kutumia silaha imepangwa kuanza kusikilizwa leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha.
Post a Comment