MAMBO KUMI YAKUMBUKA KIPINDI CHA JPM MWAKA HUU 2017 - EDUSPORTSTZ

Latest

MAMBO KUMI YAKUMBUKA KIPINDI CHA JPM MWAKA HUU 2017




Rais Dk. John Magufuli akipokelewa na Jakaya Kikwete.
RAIS Dk. John Magufuli amefanya mambo mengi ndani ya mwaka huu, lakini haya 10 yatazidi kukumbukwa na Watanzania.

BABU SEYA, PAPII KOCHA
Tukio la kuachiwa kwa wanamuziki Nguza Mbangu Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) lilitangazwa na Rais Magufuli wakati wa maadhimisho ya uhuru, Desemba 9, mwaka huu.

Rais alipotangaza msamaha kwa wanamuziki hao maarufu kuliamsha nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini.

Familia hiyo ilianza kutumikia kifungo cha maisha jela tangu Juni mwaka 2004 kwa kosa la kuwalati wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, jijini Dar es Salaam.

RELI YA KISASA
Tukio la ujenzi wa reli ya kisasa lilikuwa la kipekee kwa nchi yetu kwani Rais Magufuli alizindua rasmi ujenzi wake akasema itasafiri kwa mwendo wa kilomita 160 kwa saa.

Rais alisema Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika ambayo imeweza kujenga mradi wa reli kama hiyo kwa fedha zake za ndani.

Ujenzi wake umeanzia Dar es Salaam kwenda Morogoro na utagharimu dola za Marekani bilioni 1.29 na shughuli za ujenzi wa reli hiyo zinaendelea.

TANESCO, WIZARA ZIVUNJWE
Mwaka huu pia, Rais Magufuli alitembelea mradi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo na kuagiza majengo ya makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Maji yavunjwe.

Alitoa maagizo hayo kutokana na majengo hayo kujengwa ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro.

Majengo ya wizara tayari yamevunjwa na Tanesco inaendelea na mchakato wa ubomoaji.

MABWENI YA UDSM
Jambo jingine ambalo Rais Magufuli atakumbukwa nalo kwa mwaka huu, ni uzinduzi wa majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).

Mabweni hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 na yalijengwa chini ya mwaka mmoja na kugharimu sh. bilioni 10.

Hivi karibuni majengo hayo yaliripotiwa kuwa na nyufa, lakini Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) uliwatoa hofu wanafunzi kuwa hayana tatizo.

KUVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI
Oktoba mwaka huu, Rais Magufuli alivunja Baraza la Mawaziri na kufanya mabadiliko kadhaa.

Katika mabadiliko hayo, aliongeza wizara na mawaziri kutoka 19 hadi 21. Nafasi za manaibu mawaziri ziliongezwa kutoka 16 hadi 21.

Lengo la mabadiliko hayo ilielezwa ni kuleta ufanisi wa kiutendaji serikalini.

DAWA ZA KULEVYA
Alipoingia madarakani alitangaza kiama cha wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya na vigogo kadhaa walikamatwa kujihusisha nazo.

Februari mwaka huu, rais alimteua Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Baada ya uteuzi huo, Sianga alimhakikishia rais kuwa atapambana na dawa hizo hadi ushindi upatikane.

Agosti, mwaka huu, Rais Magufuli alimteua pia Luteni Kanali Frederick Felix Milanzi kuwa Kamishna wa Operesheni wa mamlaka hiyo ili kukoleza vizuri moto wa kukabiliana na dawa hizo nchini.

BANDARINI
Mwaka huu rais alifanya pia ziara ya kushtukiza bandarini na kukuta tena madudu mengine, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake bandarini hapo.

Safari hii alikuta magari 50 yaliyoagizwa nchini na watu wasiojulikana kwa jina la Ofisi ya Rais.

Rais Magufuli alisema magari hayo siri yake ni kubwa kwani yamekaa bandarini tangu Juni mwaka 2015 na yaliletwa pamoja na magari ya serikali.

Akahoji,“inakuwaje rais nipate taarifa za magari kufichwa lakini waziri, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) msijue?”

MADENI YA WALIMU
Desemba mwaka huu, rais alirejesha matumani ya walimu ambao kwa muda mrefu wanasumbukia madai yao bila ufumbuzi.

Akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Desemba 14, mwaka huu, mjini Dodoma, aliahidi kulipa takriban sh. bilioni 25 za madeni ya walimu.

“Ninawaahidi walimu wenzangu, mara baada ya uhakiki kuisha wale walimu ambao wanadai malipo halali watalipwa,”alisema.

Alisema kabla hajawa rais alikuwa mwalimu hivyo anazifahamu vizuri shida za walimu hivyo walimu wajisikie wana mwakilishi mzuri.

MADINI
Rais Magufuli aliunda tume mbili kuchunguza madai ya wizi na ufisadi unaodaiwa kufanywa na wawekezaji tangu walipoanza uzalishaji wa dhahabu nchini.

Ripoti ya kamati ya kwanza ilipotoka ikiongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilibaini kasoro za usimamiaji, hivyo rais alimfuta kazi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kuvunja Bodi ya Uwakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).

Ripoti ya kamati ya pili iliongozwa na Profesa Nehemia Ossoro ilibaini usafirishaji wa mchanga umepotezea taifa fedha nyingi.

Profesa Ossoro alisema fedha zilizopotea tangu mwaka 1998 ni kati ya sh. trilioni 132 hadi trilioni 380.

BOMBA LA MAFUTA
Mwaka huu ulikuwa pia na tukio la aina yake. Ni uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Bomba litapita mikoa nane, wilaya 24 na vijiji 124 na wakandarasi watatu kutoka nje wanasimamia mradi huo na kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa wananchi wa pande hizo mbili.

EDUSPORTSTZ inakutakia maandalizi mema ya siku. inakuomba kulike facebook page yetu au kufollow kupitia blog eneo la follow by email ili kutumiwa habari kwa wakati http://www.edusportstz.com ni fahari ya wasomaji
Follow web yetu na like facebook page yetu hapa kwa habari za uhakika,ni rahisi mno


Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz