CHAMA, MWALIMU, MORISS NA TOURE WAIZAMISHA TANZANIA PRISONS

SIMBA SC imeonyesha ubora wake mbele ya mashabiki wake baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwa kasi na ushindani mkubwa.

Wekundu hao wa Msimbazi walitawala mchezo kwa kiasi kikubwa tangu dakika za mwanzo na kuonyesha dhamira ya kutafuta ushindi mapema.

Simba ilianza kufungua pazia la mabao dakika ya 27 kupitia mshambuliaji wake, Morris Abraham, aliyetikisa nyavu baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Antony Mligo.

Bao hilo liliwapa nguvu wenyeji kuendelea kushambulia huku Tanzania Prisons wakionekana kupata wakati mgumu kuhimili kasi ya mchezo.

Dakika ya 42, kiungo mshambuliaji Clatous Chama aliandika bao la pili kwa Simba baada ya kutumia vizuri nafasi aliyopata ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilizidi kuwapa presha wageni huku Simba wakionekana kucheza kwa kujiamini zaidi mbele ya mashabiki wao.

Kabla ya mapumziko, Seleman Mwalimu naye aliingia kwenye orodha ya wafungaji kwa kuifungia Simba bao la tatu dakika ya 44 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Libase Gueye.

Ushirikiano wa safu ya ushambuliaji ya Simba uliendelea kuwa mwiba mkali kwa walinzi wa Tanzania Prisons waliolazimika kufanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi.

Katika dakika za mwanzo za mchezo, Simba pia ilipata penalti dakika ya 11 baada ya Salum Kimenya kumuangusha Antony Mligo ndani ya eneo la hatari.

Penalti hiyo ilipigwa na Seleman Mwalimu lakini haikuzaa matunda baada ya mpira huo kupaa juu na kuacha mashabiki wakishikwa na taharuki kwa muda mfupi.

Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Simba wakiwa mbele kwa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons, kabla ya Ismael Touré kuongeza bao la nne dakika ya 62 na kuhitimisha karamu ya mabao kwa wenyeji.

Ushindi huo unaendelea kuipa Simba nguvu katika mbio za kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

The post CHAMA, MWALIMU, MORISS NA TOURE WAIZAMISHA TANZANIA PRISONS appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/LsGPbva
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post