SIMBA WAWEKA MSIMAMO WAZI LICHA YA KUPOTEZA POINTI

LICHA ya kupata sare ya pili mfululizo dhidi ya TRA United, uongozi wa Simba kupitia Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, amesema  matokeo hayo hayajawakatisha tamaa wala kuwaondoa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba iliingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kutoa sare nyingine dhidi ya Azam FC, hali iliyosababisha kupoteza pointi nne na kuambulia mbili katika michezo miwili, jambo lililozua hofu kwa mashabiki kuhusu hatma ya ubingwa.

Akizungumzia matokeo hayo, Ahmed Ally amekiri kuwa hayakuwa ya kuridhisha, lakini amesisitiza kuwa bado kikosi hicho kina ari na dhamira ya kupambana hadi mwisho wa msimu.

“Bado mbio za ubingwa ziko wazi. Sare dhidi ya TRA haijatukatisha tamaa wala kutuondoa katika mipango yetu, tunaendelea kupambana,” amesema.

Ameongeza kuwa mchezo dhidi ya TRA ulikuwa mgumu, akieleza kuwa hali hiyo ni ya kawaida kwa timu zinazowania ubingwa kukutana na changamoto kama hizo katika msimu.

“Tunafahamu mechi ya TRA ni ngumu, na kwa wanaowania ubingwa lazima wakutane na matokeo ya aina hii,” ameongeza.

Amewataka mashabiki wa Simba kuendelea kuwa na imani na timu yao licha ya matokeo hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kuelekeza nguvu kwenye mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Dodoma Jiji.

“Ni mechi ngumu ya mtoano, ukipoteza unaondolewa. Tunaamini tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kuchukua ubingwa,” amesema.

Simba inatarajiwa kushuka dimbani Jumapili, Aprili 12, 2026, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Dodoma Jiji FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha

The post SIMBA WAWEKA MSIMAMO WAZI LICHA YA KUPOTEZA POINTI appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/6mTzHxl
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post