HATMA ya Simba na Yanga sasa ipo mikononi mwa mwamuzi kutoka Kenya, Dickes Mimisa Nyagrowa, atakayesimamia fainali ya Kombe la Muungano inayosubiriwa kwa hamu kubwa visiwani Zanzibar.
Uamuzi huo wa Kamati ya Mashindano umeongeza presha na mjadala kwa mashabiki wa soka, wakisubiri kuona nani ataibuka bingwa katika Kariakoo Derby hiyo ya kusisimua.
Awali, hadi kufikia jioni ya Aprili 28, 2026, kamati hiyo ilikuwa bado haijatangaza rasmi mwamuzi wa pambano hilo lililopangwa kuchezwa Aprili 29, 2026 saa 2:15 usiku katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Hali hiyo iliibua sintofahamu kwa wadau wa soka kabla ya uamuzi wa mwisho kuwekwa wazi.
Baadaye usiku, kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Nyagrowa alitangazwa rasmi kuwa mwamuzi wa kati wa mchezo huo.
Mwamuzi huyo raia wa Kenya ana kibarua kizito cha kusimamia mechi yenye ushindani mkubwa kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga.
Katika kusaidia majukumu yake, Nyagrowa atasaidiwa na waamuzi kutoka Zanzibar ambapo Ally Mbwana atakuwa msaidizi wa kwanza, huku Yusuf Shombe akichukua nafasi ya msaidizi wa pili.
Aidha, Is’haka Mwalile kutoka Tanzania Bara atakuwa mwamuzi wa akiba, wakati Ramadhan Kibo atasimamia majukumu ya kamishna wa mechi hiyo.
Nyagrowa anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa kimataifa, akiwa tayari amechezesha mashindano mbalimbali ya Afrika ikiwemo AFCON za vijana na wakubwa pamoja na CHAN.
Uzoefu huo unampa nafasi ya kusimamia mchezo huo kwa umakini mkubwa, huku macho yote yakielekezwa kwake kuhakikisha haki inatendeka dimbani.
Wakati huo huo, imeelezwa kuwa mgeni rasmi wa fainali hiyo atakuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kufuatia mabadiliko ya awali ambapo ilitarajiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel John Nchimbi, ndiye angehudhuria kabla ya ratiba kubadilika.
The post NI DAKIKA 90 TU, MKENYA AAMUA NANI MBABE appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/l3ps12I
via IFTTT
Post a Comment