MIDO AINGIA ANGA ZA AZAM FC

MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, wameanza harakati za kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao na kwa sasa wanafuatilia kwa ukaribu uwezekano wa kumpata kiungo mkabaji wa Singida Black Stars, Khalid Habib Idd ‘Gego’.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Gego anawindwa na Azam kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la kiungo la timu hiyo, licha ya JKT Tanzania kuanza pia mchakato wa kuhakikisha inaipata saini yake mwishoni mwa msimu huu.

Soka la Bongo linatambua Gego anawindwa na timu hizo kutokana na ubora alionao, ingawa, chanzo kinaeleza Azam FC ndiyo inayopewa nafasi zaidi ya kumsajili mchezaji huyo, ikiwa atashindwana na waajiri wake hao wa sasa Singida Black Stars.

“JKT Tanzania ndio timu ya kwanza kumhitaji tangu dirisha dogo la Januari 2026, japo kutokana na umuhimu wake kikosini ilikuwa ngumu kwa benchi la ufundi kumwachia aondoke kirahisi, ingawa, Azam pia imeingilia kati,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema licha ya JKT kuonyesha nia ya wazi ya kumhitaji tangu mwanzo, lakini Azam imeweka kiasi kikubwa pia cha fedha kwa ajili ya kumpata kwa msimu ujao, jambo ambalo huenda likamshawishi kiungo huyo kujiunga na kikosi hicho.

“Singida inafanya mazungumzo na menejimenti ya mchezaji mwenyewe ili kumwongezea pia mkataba mpya na kuboresha baadhi ya masilahi yake muhimu, japo hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kwa pande zote mbili,” kilisema chanzo hicho.

Gego alijiunga na Singida Black Stars msimu wa 2023-2024, akitokea KMKM FC ya Zanzibar na mkataba wake wa miaka miwili aliousaini unafikia tamati mwisho wa msimu huu wa 2025-2026, jambo linaloziingiza vitani timu nyingine pia.

Akiwa na KMKM, nyota huyo alikuwa kivutio zaidi kutokana na uwezo wake mkubwa, ambapo kabla ya kujiunga na kikosi cha Singida msimu wa 2022-2023, alishinda tuzo mbili, ambazo ni za kiungo bora na mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

The post MIDO AINGIA ANGA ZA AZAM FC appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/RcplVIf
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post