CHAMPIONSHIP SASA NI MWENDO MDUNDO

UHONDO wa Ligi ya Championship unaendelea wikiendi hii kwa mechi tano kupigwa leo Jumamosi na nyingine pia tatu kesho Jumapili, kuhitimisha raundi ya 23, ikiwa ni lala salama kwa kila timu kujiwekea mazingira bora.

B19 FC yenye kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-0, mechi ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar, itakuwa na kibarua kingine kigumu cha kupambana na vinara wa ligi hiyo, Geita Gold, iliyotoka kuitembezea kichapo cha mabao 6-1, Hausung FC kutoka Njombe.

Timu hiyo zamani Tanesco, itakuwa kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF, Kigamboni, jijini, Dar es Salaam, kuikaribisha Geita Gold, ambayo kwa sasa imekuwa na mwenendo mzuri katika mechi za Ligi ya Championship, chini ya Kocha, Zubery Katwila.

B19 FC iko nafasi ya 12 katika msimamo na pointi 21, baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 11, kati ya 22 iliyocheza na safu yake ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 20 na kuruhusu 35.

Geita Gold ni vinara wa Ligi ya Championship ikiwa na pointi 55 baada ya kushinda mechi 17, ikitoka sare nne na kuchapwa moja, ikifunga mabao 44 na kuruhusu 13, ikipambana kurejea Ligi Kuu, baada ya kushuka msimu wa 2023-2024.

Msimu wa 2024-2025 ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.

Geita ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.

Kwenye Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, Hausung FC iliyotoka kuchapwa mabao 6-1, dhidi ya Geita Gold, wiki iliyopita, inarejea nyumbani kucheza na Kagera Sugar, yenye kumbukumbu nzuri ya kutoka kuichapa B19 FC mabao 2-0.

Hausung FC iliyopanda daraja msimu huu, inashika nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tatu tu, sare mbili na kupoteza 17, kikiwa kimefunga mabao 15 na kuruhusu 43.

Kwa upande wa Kagera Sugar, katika mechi 22, imeshinda 16, sare nne na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya pili na pointi 52, nyuma ya vinara Geita Gold na inapambana kurejea ligi kuu, baada ya kushuka msimu wa 2024-2025.

Kagera iliyodumu Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, baada ya kukusanya pointi zake 23.

Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ana kazi ya kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.

Kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani, Transit Camp iliyochapwa kwa mabao 2-1, dhidi ya maafande wenzao wa Polisi Tanzania, itaendelea kubakia uwanjani hapo kuikaribisha African Sports, iliyotoka kuichapa Barberian FC bao 1-0.

Songea United iliyoichapa Bigman FC bao 1-0, mechi ya mwisho, itaendelea kubakia kwenye Uwanja wa Majimaji, uliopo mjini Songea, mkoani Ruvuma, kuikaribisha Mbeya Kwanza, iliyotoka pia kushinda mabao 4-1, dhidi ya KenGold FC.

Mechi ya mwisho leo Jumamosi, itapigwa kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi na baada ya Polisi Tanzania kuichapa maafande wenzao wa Transit Camp mabao 2-1, itaikaribisha Barberian FC, inayoburuza mkiani mwa msimamo na pointi zake 10.

Polisi msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10 katika ligi hiyo na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 na imefunga mabao 44 na kuruhusu 33.

Kikosi hicho kinachopambana ili kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 25, msimu huu kiko nafasi ya nne na pointi 45, kikishinda mechi 13, kikitoka sare sita na kupoteza tatu tu.

Kwa upande wa Barberian FC zamani Kiluvya United, msimu huu umekuwa ni mgumu zaidi kwa timu hiyo na inashika nafasi ya 16, ikiburuza mkiani na pointi 10, baada ya kushinda mechi moja tu, sare saba na kupoteza 14 kati ya 22.

Uhondo wa ligi hiyo utaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi tatu kupigwa na Mbuni FC iliyochapwa na Gunners FC ya Dodoma mabao 3-2, itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini, Arusha kuikaribisha Stand United ‘Chama la Wana’.

Mbuni FC inayoshika nafasi ya sita na pointi 38, imeshinda mechi 12, sare mbili na kupoteza nane, huku kwa upande wa Stand United yenye kumbukumbu ya kuchapwa na TMA FC mabao 4-2, ikiwa nafasi ya 13, baada ya kukusanya pointi zake 20.

Kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Chunya, jijini, Mbeya, KenGold iliyochapwa na Mbeya Kwanza mabao 4-1, mechi iliyopita, itabakia nyumbani kwa kukikaribisha Bigman FC, kilichotoka pia kuchapwa na Songea United bao 1-0.

Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu, baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.

Hata hivyo, KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu Bara na kushuka daraja msimu wa 2024-2025, ikimaliza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar, iliyomaliza ya 15 na pointi 23.

Baada ya TMA FC kuichapa Stand United mabao 4-2, itakuwa uwanja wake wa nyumbani kuikaribisha Gunners FC kutoka jijini, Dodoma, yenye kumbukumbu nzuri, baada ya mechi iliyopita kushinda mabao 3-2, dhidi ya Mbuni FC ya Arusha.

Kocha wa African Sports, Ally Salimu Mdoe ‘Bai’, amesemamalengo ya timu hiyo kwa sasa ni kupambana katika mechi nane zilizobakia, ili kukitoa kikosi hicho katika nafasi za kucheza mtoano (Play-Off), licha ya ushindani pia mkubwa uliopo.

The post CHAMPIONSHIP SASA NI MWENDO MDUNDO appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/okj4NJF
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post