DURU LA PILI MOTO, DEPU ARUDI, YANGA YAANZA VITA RASMI

KUREJEA kwa mshambuliaji wa Yanga, Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’, kumekipa kikosi hicho nguvu mpya na kuibua matumaini makubwa kuelekea duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nyota huyo alikuwa akisumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje katika baadhi ya mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza, hali iliyopunguza makali ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Hata hivyo, sasa Depu amepona na kurejea rasmi kikosini, jambo ambalo limeongeza chachu ndani ya timu huku wachezaji na benchi la ufundi wakionekana kuwa na morali ya juu.

Akizungumza kuhusu hali ya kikosi, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi, akiwemo Depu, ni ishara njema kwa timu yao kuelekea hatua inayofuata ya ligi.

“Ligi irudi sasa, tumetimia. Wachezaji wetu waliokuwa majeruhi wamerejea na tayari wameanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu,” amesema Kamwe.

Yanga tayari imeanza mazoezi makali ikijiandaa na mchezo wao wa kwanza baada ya mapumziko ya FIFA Series, wakilenga kuanza kwa ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani.

Katika mchezo huo, Yanga inatarajiwa kukutana na Tanzania Prisons, Jumamosi, Aprili 4, 2026, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, huku macho na masikio ya mashabiki yakielekezwa kuona kiwango cha Depu baada ya kurejea dimbani.

The post DURU LA PILI MOTO, DEPU ARUDI, YANGA YAANZA VITA RASMI appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/bT8rQjC
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post