BEKI wa Dodoma Jiji FC, Abdi Banda, amesema kuondolewa kwa timu yao katika michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB na Simba kumewaumiza, lakini tayari wameanza kujiandaa kulipa kisasi katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Dodoma Jiji waliondoshwa kwenye mashindano hayo jana baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba, matokeo yaliyowafanya washindwe kufuzu hatua ya robo fainali.
Banda amesema wameyakubali matokeo bila kulaumiana, akisisitiza kuwa walicheza vizuri kwa sehemu kubwa ya mchezo kabla ya kupoteza umakini katika dakika za mwisho, jambo lililoigharimu timu yao.
“Tumekubaliana na matokeo na sasa tunageukia kilicho mbele yetu. Tuna mechi nyingine dhidi yao katika mzunguko wa pili jijini Dar es Salaam, na safari hii hatutakuwa tayari kufungwa tena,” alisema Banda.
Amesema kuwa kwao kupoteza dhidi ya Simba si jambo la kushangaza sana, lakini akabainisha kuwa presha huwa kubwa zaidi kwa wapinzani wao wanapopoteza.
“Kwa upande wetu, kufungwa si jambo kubwa sana, lakini wao wakifungwa inakuwa stori kubwa. Tunakumbuka tulipata sare Dodoma, na sasa tunaenda Dar es Salaam kufuata pointi tatu,” ameongeza.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuchezwa Mei 24, 2025, katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam, ambapo Simba watakuwa wenyeji.
The post DODOMA JIJI WAFICHA MAUMIVU, WAWEKA NIA YA KULIPA KISASI DHIDI YA SIMBA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/xL4jsSl
via IFTTT
Post a Comment