NAHODHA wa Simba SC, Rushine De Reuck, amevunja ukimya baada ya kuongeza mkataba wake kuendelea kuitumikia timu hiyo ya Msimbazi, akieleza kuwa bado ana deni kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo na anaamini bado ana mengi ya kuifanyia Simba.
Beki huyo raia wa Afrika Kusini amesema tangu siku ya kwanza alipowasili ndani ya kikosi hicho alipokelewa kwa upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki na uongozi wa klabu, jambo lililomfanya ajisikie yupo sehemu sahihi ya kuonyesha na kuendeleza kipaji chake cha soka.
Amesema uamuzi wa kuongeza mkataba una maana kubwa kwake binafsi kwani unaonyesha imani kubwa aliyopewa na viongozi pamoja na mashabiki wa Simba ambao wameendelea kumuunga mkono tangu alipojiunga na timu hiyo.
Rushine amefichua kuwa mtu wa kwanza kumpa taarifa kuhusu kuongeza mkataba huo alikuwa ni mama yake, ambaye alifurahia sana kusikia habari hizo kwa kuwa anaamini mwanawe yupo katika mazingira mazuri ya kukuza kipaji chake cha soka.
Nahodha huyo amesema katika kipindi chote alichokuwa akiitumikia Simba amekuwa akijitahidi kuonyesha kiwango bora uwanjani, lakini bado hajawahi kuridhika na kiwango chake kwani kila anapomaliza mechi hujifanyia tathmini binafsi ili kubaini mambo anayopaswa kuyaboresha.
“Nimekuwa katika kiwango bora lakini kila nikimaliza mechi huwa najifanyia tathmini kuona ni kitu gani natakiwa kuboresha. Unaweza kusema najiamini kwa sababu nimecheza soka la Afrika kwenye ushindani mkubwa,” amesema Rushine.
Ameongeza kuwa lengo lake tangu ajiunge na Simba ni kucheza soka la kiwango cha juu na kusaidia timu kufikia malengo yake, akisisitiza kuwa kila mchezaji ndani ya kikosi hicho anapaswa kutoa mchango mkubwa kwa manufaa ya klabu.
Kwa mujibu wa Rushein, Simba ni klabu kubwa yenye historia na matarajio makubwa, hivyo jukumu lao kama wachezaji ni kupambana kwa nguvu zote ili kurejesha heshima ya timu hiyo kwa kutwaa mataji, hasa ikizingatiwa kuwa imepita muda tangu klabu hiyo ishinde ubingwa wa ligi.
“Simba ni timu kubwa na lazima tupambane. Wachezaji wengi wenye ubora wanatamani kucheza hapa, hivyo sisi tunapaswa kutoa kilicho bora na kuhakikisha tunaipa Simba ubingwa,” amesema beki huyo.
The post RUSHINE ALAA KIAPO KWA SIMBA, SABABU ZA KUONGEZA MKATABA appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/vacr07Q
via IFTTT
Post a Comment