REKODI ZAFICHUA USHINDANI MKALI KARIAKOO SERBY

USIKU wa deni haukawii kukucha! Hatimaye siku ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini imewadia, kwa kushuhudia pambano la Kariakoo Derby kati ya Yanga SC na Simba SC.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa saa 2:15 usiku katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, huku Yanga wakiwa wenyeji wa pambano hilo linalobeba hisia, presha na historia kubwa kwa pande zote mbili.

Kwa miaka kadhaa sasa, Kariakoo Derby imeendelea kuwa kitovu cha ushindani mkali ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2017 hadi 2026, watani hao wa jadi wamekutana mara 16 katika mechi za ligi, zikidhihirisha namna ambavyo wamekuwa wakipishana kwa karibu katika ubora.

Katika idadi hiyo ya michezo 16, Yanga imeibuka na ushindi mara sita,  Simba ikishinda mara tatu, wakati michezo saba ikimalizika kwa sare. Hali hiyo inaonyesha wazi kuwa licha ya Yanga kuwa na faida ndogo ya matokeo, derby hiyo imekuwa na ushindani wa hali ya juu usiotabirika kirahisi.

Upande wa mabao, Yanga imefunga jumla ya mabao 17 dhidi ya 11 ya Simba. Hata hivyo, Yanga pia imefungwa mabao 17  idadi sawa na ambayo Simba imefungwa katika kipindi hicho.

Jambo linalosisitiza usawa wa ushindani wao kila wanapokutana. Kwenye safu ya ulinzi, Yanga imecheza mechi saba bila kuruhusu bao (clean sheet), wakati Simba ikiwa na clean sheet sita.

Kwa upande wa nidhamu, derby hiyo imeendelea kuonyesha ugumu wake ndani ya uwanja. Yanga imeonyeshwa jumla ya kadi 41 za njano na kadi moja nyekundu, huku Simba ikipata kadi 48 za njano bila kuonyeshwa kadi nyekundu katika kipindi hicho cha miaka tisa. Takwimu hizi zinaakisi presha na mapambano makali yanayoambatana na kila pambano lao.

Kwa ujumla, takwimu hizi zinaweka wazi kuwa licha ya Yanga kuwa na makali kidogo katika ushindi wa miaka ya karibuni, Kariakoo Derby imeendelea kuwa vita ya heshima na kujituma, ambapo kila timu imekuwa na nyakati zake za kung’ara.

Hivyo, macho na masikio ya mashabiki kwa mara nyingine tena yataelekezwa Zanzibar kushuhudia nani ataandika sura mpya ya historia ya watani wa jadi.

The post REKODI ZAFICHUA USHINDANI MKALI KARIAKOO SERBY appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/54KDa09
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post