KIUNGO wa Simba SC, Ellie Mpanzu, ameanza kurejea taratibu katika ubora wake na kuondoa presha iliyokuwa ikimkabili baada ya kushuka kwa kiwango katika kipindi cha hivi karibuni.
Hatua ya kuanza kutoka benchi katika baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaonekana kuwa mwanzo mpya kwake, huku ikimpa nafasi ya kujipanga upya bila mzigo mkubwa wa matarajio.
Kwa muda, kiwango cha Mpanzu kilikuwa kikizua maswali miongoni mwa mashabiki wa Simba, wengi wakihitaji kuona mchango wake ukiwa thabiti zaidi.
Hata hivyo, mabadiliko ya kiufundi yaliyofanywa na benchi la ufundi, linaloongwa na Kocha Steve Barker yanaonekana kumpa nafasi ya kurejesha kujiamini na kurudi kwenye ubora wake wa zamani hatua kwa hatua.
Kwa mujibu wa kocha Barker, kila anapopata nafasi ya kucheza, Mpanzu ameanza kuonyesha dalili za kurejea katika kiwango chake bora.
Amesema akiingia kama mchezaji wa akiba, amekuwa akileta nguvu mpya, ubunifu na kasi ambayo imekuwa ikibadilisha mwelekeo wa mchezo kwa nyakati tofauti.
“Mfano halisi wa mabadiliko hayo ni bao lake dhidi ya Singida Black Stars, alionyesha utulivu, umakini na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi sahihi ndani ya eneo la hatari.
Bao hilo limekuwa ishara kwamba bado ana nafasi kubwa ya kuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi hicho,” amesema kocha huyo.
Kocha Steve Barker ameonekana kutumia mbinu ya usimamizi wa mchezo kwa umakini mkubwa kwa Mpanzu, akihakikisha anapata muda sahihi wa kucheza huku akilinda afya yake ya kimwili na kiakili. Lengo likiwa ni kumrejesha katika kiwango cha juu kwa faida ya timu nzima.
Wadau wa soka wanaona kuwa hatua ya kumpa nafasi ya kuanza kutoka benchi si adhabu, bali ni mkakati wa kumjenga upya ili arejee akiwa imara zaidi. Ni mbinu ambayo mara nyingi hutumika kwa wachezaji wanaopitia changamoto ya kiwango, ili kuwapa nafasi ya kurejesha makali yao bila presha kubwa.
Kwa mwendo huu, dalili zinaonyesha kuwa Mpanzu yuko njiani kurejea katika ubora wake kamili na ataendelea na kasi hii, si mashabiki wa Simba pekee watakaofurahia, bali hata wapinzani wataanza kuwa na sababu ya kuwa na hofu kutokana na mchango wake unaotarajiwa katika michezo ijayo.
The post MPANZU AIBUKA UPYA, WAPINZANI WAANZA KUPATA HOFU appeared first on Soka La Bongo.
from Soka La Bongo https://ift.tt/SOzu6Zm
via IFTTT
Post a Comment