MBIO ZA ALAMA 12 ZAMUWEKA PEDRO KWENYE WAKATI MGUMU

RATIBA ngumu ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeanza kumweka kwenye wakati mgumu Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, wakati timu hiyo ikiwa na jukumu la kusaka alama 12 muhimu katika michezo minne ya ugenini.

Kocha huyo amesema msongamano wa ratiba umekuwa changamoto kubwa kwa kikosi chake, kwani wanapaswa kucheza mechi kila baada ya siku mbili huku wakilazimika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Pedro ameeleza kuwa pamoja na ugumu huo, benchi la ufundi linaendelea kufanya maandalizi ya kina ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa tayari kimwili na kiakili kukabiliana na kila mchezo unaowakabili katika kipindi hiki kigumu.

Katika ratiba hiyo, Yanga itaanza safari yake kwa kukutana na Tanzania Prisons katika mchezo utakaochezwa Alhamisi, Machi 12, kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo mwingine mkali dhidi ya Azam FC utakaopigwa kwenye dimba la Azam Complex.

Baada ya mchezo huo, mabingwa hao watasafiri tena kuelekea Tabora ambapo watakabiliana na TRA United katika mchezo uliopangwa kuchezwa Machi 18, kabla ya kumaliza mzunguko huo wa mechi za ugenini kwa kukipiga dhidi ya Mtibwa Sugar Machi 21.

Licha ya ratiba hiyo kuwa ngumu, Pedro anaamini kikosi chake kina uwezo wa kupambana na kupata matokeo chanya ikiwa wachezaji wataendelea kuonyesha nidhamu, kujituma na kuzingatia maelekezo ya benchi la ufundi.

Amesisitiza kuwa malengo ya Yanga ni kuhakikisha wanapata alama zote muhimu katika michezo hiyo ili kuendelea kuimarisha nafasi yao katika mbio za ubingwa wa ligi msimu huu.

The post MBIO ZA ALAMA 12 ZAMUWEKA PEDRO KWENYE WAKATI MGUMU appeared first on Soka La Bongo.



from Soka La Bongo https://ift.tt/G3DhRW0
via IFTTT

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post